Maximo apewa mkataba mpya

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) jana limetangaza rasmi kuwa limemuongezea mkataba mwingine wa mwaka mmoja wa kuifundisha timu ya taifa, Taifa Stars, kocha, Marcio Maximo ambaye anatoka nchini Brazil.

Kocha wa Taifa Stars

Akizungumza jana jijini, Rais wa TFF. Leodegar Tenga alisema kuwa mkataba wa awali wa kocha huyo ambao ulisainiwa Julai 28 mwaka 2006 ulikuwa unamalizika Julai 27 na hivyo kutokana na kocha huyo kuweza kutekeleza makujumu yake kwa kiwango kikubwa wameamua kumuongezea muda huo.

Tenga alisema kuwa shirikisho hilo lilikuwa linahitaji kumpa mkataba mwingine wa miaka miwili au zaidi lakini wameshindwa kufikia maamuzi na kocha huyo kutokana na sababu binafsi alizowapa na hivyo kumuelewa.

Tenga alisema pia pamoja na sababu hizo, TFF imekubaliana na Maximo kuwa endapo itafanikiwa kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa Afrika za mwaka 2010, Maximo ataongoza benchi la ufundi wa timu hiyo.

“Tunaamini kuwa bado tunaweza kufuzu kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia na za Afrika, hivyo tumeshakubaliana nae kuwa tukifanikiwa kama ambavyo tunaamini atakuwepo katika benchi la ufundi,“ alisema Tenga.

Aliongeza kuwa katika kipindi chote ambacho Maximo amefanya kazi nao ameonyesha kutengeneza mfumo wa kisasa wa timu ya taifa kama ambavyo timu zilivyoendelea zinavyojiendesha na kuonekana kuwa na mabadiliko ya kimaendeleo.

Alisema pia katika hadidu rejea ambazo walimpatia kocha huyo wakati anajiunga na Stars walimueleza kwamba wanataka kuona timu inajengeka na hilo limeonekana kufanikiwa kwa sababu amefanikiwa kutambua vipaji vipya na kuviendelea vile alivyovikuta katika timu hiyo.

Alisema pia suala la nidhamu ambalo kocha huyo amelisimamia kwa kuamini kuwa hiyo ndio sifa muhimu kwa mchezaji bora na yeye mwenyewe amekuwa mfano kwa kulitekeleza katika kipindi chote alichokuwepo hapa nchini.

“Huwezi kuzungumzia mafanikio ya timu ya taifa bila kumtaja kocha, Stars imepiga hatua kwa kiasi kikubwa ambapo akiwa na timu tumecheza mechi 26, tumeshinda tisa, tumetoka sare michezo 11 na tumepoteza mechi sita,“ alisema Tenga.

Alisema pia hata pale timu ilipopoteza mechi iwe ya mashindano au ya kirafiki kocha huyo hajawahi kutoa visingizio na hivyo ni sababu wanataka kuiandikia serikali barua na kumpa ripoti ya nia ya kuwa naye katika kipindi kingine cha mwaka mmoja.

Maximo alisema kuwa anafurahi kuendelea kufanya kazi hapa nchini na kuongeza kuwa anajiona ni mwenye bahati kwa sababu alipokuwa anakubali jukumu la kuinoa Stars na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliona kapewa jukumu gumu sana.

Kocha huyo ni mwajiriwa wa TFF lakini analipwa mshahara na serikali kupitia wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments