Ushindi wa Cape Verde waiweka pabaya Stars

CAPE Verde juzi iliiweka pabaya timu ya taifa ya soka, Taifa Stars baada ya kupata ushindi mwingine wa bao 1-0 dhidi ya Mauritius na kujichimbia katika nafasi ya pili katika Kundi la Kwanza.

Ushindi huo umeifanya timu hiyo kutoka visiwani kufikisha pointi sita baada ya michezo mitatu na hivyo kuzidiwa na vinara wa Kundi la Kwanza, Cameroon katika mbio za kuelekea fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

Cameroon inaongoza kwa kuwa na pointi saba baada ya kushinda mechi mbili za kwanza (kwa mabao 3-0 dhidi ya Mauritius na mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde) na kulazimishwa sare yake ya kwanza jijini Dar es salaam na Taifa Stars Jumamosi iliyopita.

Sare hiyo iliifanya Stars, ambayo ilitoka sare ya bao 1-1 na Mauritius jijini Dar es salam na kufungwa bao 1-0 na Cape Verde mjini Prai, ifikishe pointi mbili ambazo kocha Marcio Maximo alisema Jumamosi iliyopita kuwa zitamsaidia katika kujijengea mazingira mazuri ya mechi mbili marudiano dhidi ya Cape Verde na Mauritius ili afikishe pointi nane zitakazoisaidia kuvuka kwenda raundi ya pili, ambayo itakuwa ya kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika.

”Sare ya leo ilikuwa muhimu sana,” Maximo aliwaambia waandishi baada ya mchezo na Cameroon, ” Kama tutajitahidi na kushinda mechi dhidi ya Cape Verde na Mauritius tutafikisha pointi saba.

”Lakini itatubidi tufanye vizuri katika mechi ya Cameroon kwanza, ndipo tuwe na nafasi ya kusonga mbele.”

Lakini, matumaini hayo sasa yatabakia mikononi mwa Cape Verde, ambayo inarudiana na Mauritius mjini Praia wiki hii baada ya ushindi huo wa Jumapili uliotokana na bao la penati lililofungwa na Eduardo ‘Dady’ Gomes katika kipindi cha kwanza.

Iwapo Cape Verde itaishinda tena Mauritius, itafikisha pointi tisa na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa mshindi wa pili wa Kundi la Kwanza na hivyo kuiacha Stars ikihaha kusaka nafasi ya mshindi bora wa tatu.

Taifa Stars ilionyesha kandanda safi la kuvuruga mbinu za Cameroon, ambayo imeshatwaa ubingwa wa Afrika mara nne na kufuzu mara kwa mara kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Safu ya kiungo ilicheza vizuri kutibua mbinu za wageni waliokuwa wamesheheni wachezaji wanaosakata soka Ulaya, lakini pia ikaanzisha vizuri mashambulizi ya kushtukiza ambayo nusura yazae mabao mwishoni mwa mchezo wakati Cameroon ikionekana kuanza kuchoka.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments