Bendera, wadau waipongeza Stars

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera ameungana na wadau mbalimbali wa mchezo wa soka nchini kuipongeza timu ya soka ya taifa, Taifa Stars kwa kucheza vizuri katika mechi yake dhidi ya timu ya taifa ya Cameroon, ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana wakati ilionekana dhaifu kabla ya mchezo.

Hata hivyo wadau hao kwa nyakati tofauti walisema kuwa wachezaji wa Stars walitakiwa kuongeza juhudi ili kuwapa raha zaidi Watanzania kwa kufunga mabao na kurejesha matumaini ya kufuzu kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika iliweza kuibana na kutoka suluhu na Cameroon katika mchezo wake wa tatu wa kundi hilo la kwanza uliofanyika kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa.

Bendera ambaye aliwahi kuwa kocha wa timu hiyo alisema kuwa Stars waliweza kuonyesha mchezo mzuri na kuwamudu wapinzani wao mwanzo hadi mwisho wa mchezo huo bila ya kuwa hofu yoyote.

“Wengi hawakutegemea matokeo haya kutokana na ubora wa timu tuliocheza nayo, tunawapongeza vijana wetu kwa mchezo mzuri waliouonyesha, hakika wamefanya vizuri“, alisema bendera.

Alisema kuwa kiwango hicho kilichochezwa na wachezaji hao kimefungua ukurasa mpya wa nchi yetu kurejea katika medani za soka za kimataifa na kufanya maajabu zaidi.

Aliwataka pia wachezaji wa Stars kujituma zaidi na kuongeza umakini hasa upande wa washambuliaji ambao wanatakiwa kumalizia nafasi wanazopata kwa kupachika mabao.

Wakizungumza na Nipashe jana baadhi ya wapenzi wa soka wakiwemo wachezaji wa zamani wamesema kuwa Stars imeonyesha uhai na matumaini kwamba wanaweza ila wanaangushwa na safu ya ushambuliaji.

“Kwa kweli tunawapongeza wachezaji pamoja na kocha wao kwa kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo wa leo (juzi) na kufanikiwa kuibana Cameroon ambayo wengi waliipa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi,“ alisema Daudi Kanuti Afisa Utawala wa Chama cha soka wilaya ya Ilala, (IDFA).

Ramadhani Kampira alisema kuwa anawapongeza makocha na wachezaji kwa kubadilika na kuwapa matumaini Watanzania juu ya timu hiyo na kushauri kwamba safu ya ushambuliaji inatakiwa kubadilika na kuonyesha uhai wa kufunga.

“Sare tuliyopata kwa Cameroon ni kama ushindi, lakini kwa jinsi tulivyowabana wakali wale ilikuwa tushinde si chini ya mabao 2-0, ila udhaifu wa washambuliaji ni tatizo na kocha anawajibika kuendelea kufanya marekebisho kabla ya kurudiana na wababe hao,“ alisema Kampira.

Naye Saleh Hilal alisema kuwa hatupaswi kukata tamaa na badala yake watu wote wanatakiwa kuipa ushirikiano Stars utakawaongezea juhudi katika mechi zilizobakia kama walivyofanya juzi kwa Cameroon.

Stars ambayo kwa sare hiyo ya juzi imefikisha pointi mbili, italazimika kushinda mechi zake tatu zilizosalia ikiwemo ya marudiano na Cameroon itakayofanyika Jumamosi katika jiji la Yaounde.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments