Stars yaitoa kamasi Cameroon

Eto’o, Song wafichwa Dar

Misri yapigwa bao Malawi

Rwanda yaiua Morocco 3-1

Kenya, Uganda zashinda

TIMU ya soka ya Taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’ jana ilicheza soka la ‘kikubwa’ na kufanikiwa kuwazima nyota wa Cameroon waliotua nchini kwa kishindo wakiongozwa na Samuel Eto’o Fils anayeichezea Barcelona ya Hispania.

Katika mchezo huo wa michuano ya awali ya Kombe la Dunia kwa fainali za mwaka 2010 huko Afrika Kusini, mbali ya Eto’o, Cameroon ilishusha wakali wake kama kipa Idriss Kameni, Rigobert Song, Geremi Ndjitap, Timothee Atouba, Modesti Mbami, Stephen Mbia, Achille Webo na wengine.

Hata hivyo, vijana wa Stars ambao asilimia 95 wanacheza soka Tanzania, ukiondoa Nizar Khalfan na Danny Mrwanda wanaocheza Kuwait, walitandaza soka la uhakika, kiasi cha kuwaduwaza Wacameroon kwenye Uwanja Mpya wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa hakika, matokeo hayo hayakutarajiwa na wengi kutokana na ubora wa Cameroon inayoongoza kwa ubora wa soka Afrika, ikilinganishwa na Stars inayoshika nafasi ya 23, lakini ikiwa haitabiriki uwanjani.

Kabla ya kuivaa Cameroon, Stars ililazimishwa sare ya 1-1 na Mauritius kabla ya kulambwa 1-0 na Cape Verde mwishoni mwa wiki iliyopita.

Jana, wanazi wa soka wa Tanzania waliojaza uwanja mpya wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete aliyechomoka kutoka Dodoma kwenye Kikao cha NEC ya CCM, walifuwa wenye furaha isiyo kifani, kiasi cha kukufua matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zilizosalia, ikiwamo ya marudiano na Cameroon.

Mara baada ya mchezo huo, kocha Otto Pfister alishindwa kujizuia kuuonyesha mshangao wake kuhusiana na soka ya Tanzania.

Naye Eto’o, hakuweza kuamini kama Tanzania haina mchezaji anayecheza soka ya kulipwa barani Ulaya.

“Ni soka maridadi sana, wachezaji wana vipaji. Haiingii akilini kuona nchi hii haina wachezaji wa kulipwa Ulaya. Wanastahili kucheza,” alisema bila kutaja wachezaji anaodhani wapo katika kiwango cha kucheza Ulaya.

Wakati Stars ikijitutumua na kuwafunika Wacameroon, Malawi iliendelea kuonyesha maajabu ya soka, baada ya kuwazamisha mabingwa watetezi wa soka barani Afrika, Misri kwa bao 1-0 huko Blantyre, Malawi.

Bao pekee katika mchezo huo wa Kundi la 12 lilifungwa na Chiukepo Msowoya katika dakika za majeruhi. Ushindi huo umezidi kuiimarisha Malawi kileleni kwani katika mchezo wa kwanza iliishinda Djibouti kwa mabao 8-1.

Nayo Rwanda, ikicheza kwa kujiamini kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali nchini Rwanda, iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Morocoo, mashujaa wakiwa Elias Ntaganda, Bogota Labama na Olivier Karekezi waliopiga mabao. Morocco ilipata bao la kufutia machozi mfungaji akiwa Youssef Safri.

Jijini Nairobi, Kenya, mshambuliaji wa Rennes ya Ufaransa, Dennis Oliech aliifungia nchi yake bao moja, huku jingine likipigwa na McDonald Mariga, na hivyo kuizamisha Zimbabwe kwa mabao 2-0. Wiki iliyopita, Oliech aliifungia Kenya mabao yote mawili dhidi ya Namibia katika ushindi wa 2-0.

Furaha ya ushindi ilikwenda pia kwa Uganda iliyoizamisha Angola kwa bao mabao 3-0. Ilipata mabao kupitia kwa wakali Eugene Sepuya, Andrew Mwesigwa na Dan Wagaluka,.

Eric Anthony Mkuti [[email protected]]

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments