Rais wa TFF Tenga agawa majukumu mazito kwa Stars

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewapa majukumu mazito mabeki Nadir Haroub “Cannavaro’ na Salum Sued ya kuhakikisha wanamdhibiti mshambuliaji mahiri wa Cameroon, Samuel Eto’o.

Tenga alitoa maagizo hayo jana na kuwataka wachezaji hao kuhakikisha wanalala na kuota jinsi ya kumkaba Eto’o na kuhakikisha Cameroon haitoki na ushindi kwenye ardhi ya Tanzania.

“Najua mechi ni ngumu, lakini ni wajibu wenu kutoa msukumo muone raha kucheza na wachezaji wenye majina, ni mechi muhimu sana ya kuuza soko lenu la mpira,”alisema Tenga wakati akizungumza na wachezaji hao kambini kwao jana kwenye hoteli ya F&J Anex jijini Dar es Salaam.

”Ulimboka jukumu lao ni kumdhibiti Song, waonyesheni kuwa mnao uwezo, na mseme hayo kwa vitendo uwanjani ni nafasi nzuri ya kujijengea jina…. hakikisheni kesho mnatoka mkiwa mmeandika historia ya kuwafunga Cameroon,” alisema.

”Ingieni uwanjani, angalieni umati wa watu ambao umekuja kuwapa sapoti, ndani ya mioyo yenu semeni tutawapeni raha, na mhakikishe mnawapa raha kweli mashabiki, msiwatoe vichwa chini, nawaambieni mtakapofanya vizuri mkawafunga nchi itawaka moto”.

“Ni mechi muhimu sana kwenu, na ili mfuzu raundi ya pili ni lazima muwafunge Cameroon, uwezo wa kuwafunga mnao mkiwa na nia, mliwafunga Burkina Faso hapa nyumbani na baadae nyumbani kwao, wakati juzi Burkina Faso imewafunga Tunisia, uwezo mnao…..” alisema.

Makosa mliyofanya kwenye mechi ya Mauritius najua tatizo lilikuwa ni umaliziaji, naamini limeshafanyiwa kazi mechi ya kesho hatutegemei kuona tena makosa haya, ingieni mkiwa na lengo la kushinda na kufuzu sio kama timu kupata mafunzo ili uwe kwenye nafasi nzuri ni lazima uhakikishe una point 10 katika kundi lako, mkiwa na nia na mkajituma kwa dhati naamini pointi 10 zitaweza kupatikana, alisema Tenga.

Stars leo itaingia uwanjani ikiwa ni mechi yake ya tatu ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia na Afrika mwaka 2010.

Katika mechi ya kwanza Stars ilitoka sare ya bao 1-1 na Mauritus kabla ya kulazwa bao 1-0 na Cape Vede wiki iliyopita.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments