Selikali yaidai posho TFF

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limelalamikiwa kwa kuizungusha serikali na kushindwa kuilipa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Sh39milioni ili iwalipe wajumbe wake posho za vikao.

Wajumbe hao kutoka wizara hiyo, wameilalamikia TFF kwa kushindwa kuwalipa malimbikizo ya posho zipatazo Sh milioni 39 kwa ajili ya vikao vya maandalizi ya mechi ya Taifa Stars dhidi ya Mauritius.

Mechi hiyo ya kufuzu ya Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika ilifanyika wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Maandalizi ya mechi hiyo yalifanywa na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ambayo imeunda kamati kuu ambayo imefikia hadi kusimamia uchapishaji na uuzaji wa tiketi kwa ajili ya mechi za Taifa Stars.

Kamati hiyo pia imeunda kamati ndogo ambazo ni pamoja na ya ulinzi na usalama, ya habari pamoja na ufundi na usimamizi wa uwanja ambazo wajumbe wake wataka walipwe posho za vikao mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo.

Habari zinasema kuwa TFF imekuwa ikiwayumbisha ikitaka ufafanuzi wa kina.

Mtoa habari kutoka kamati mojawapo alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa kitendo cha TFF kuwazungusha kutoa fedha hizo kinawakatisha tamaa na hasa kutokana na kazi kubwa waliyofanya wakati wa mandalizi ya mechi hiyo.

Inadaiwa kuwa TFF imeshangazwa na madai hayo ya kamati kwani kwao suala la wajumbe kulipana posho ni msamiati mpya ambao hawajapata kuusikia kutokana na mechi walizokuwa wakisimamia wao wenyewe.

“Tulikaa vikao vingi sana kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo, kuna wajumbe wanatakiwa walipwe Sh300,000 na wengine Sh100,000 kutegemeana na kila kamati ilivyokutana, lakini tunashangazwa na TFF kwa kuwa wagumu kutoa fedha hizo,” alisema mtoa habari huyo kutoka wizarani.

Katika mechi hiyo, mapato yaliyopatikana yalikuwa Sh175milioni , huku wachezaji wa Stars wakiambuliwa Sh17milioni .

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments