Maulid Dilunga hatunaye tena

MCHEZAJI wa zamani wa Yanga na timu Taifa Stars, Maulid Dilunga amefariki dunia juzi usiku kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya moyo na ini.

Akizungumza jijini jana, mdogo wa marehemu, Abbas Dilunga ambaye alikuwa akiichezea Simba na Taifa Stars, alisema kaka yake aliugua kwa muda wa miezi mitatu na alilazwa katika Hospitali ya Amana, Muhimbili na baadaye alirudishwa nyumbani hadi mauti ilipomfika juzi.

”Kaka aliugua kwa takriban miezi mitatu na alilazwa katika Hospitali ya Amana, akahamishiwa Muhimbili na kabla ya kurudishwa nyumbani kwake Vingunguti,” alisema Dilunga.

Alisema marehemu huyo aliyejizolea sifa kubwa nchini kutokana na uwezo mkubwa wa kuwatoka mabeki na kufunga mabao alitarajia kuzikwa jana Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa mdogo huyo wa marehemu, Dilunga amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 62, ameacha mke na watoto sita.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments