Maximo hana jipya Stars

Baadhi ya mashabiki wa soka nchini wamesema kuwa uwezo wa Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo umefika mwisho na hana jipya katika kuibadili timu hiyo.

Hatua hiyo ya mashabiki imekuja baada ya timu hiyo kuvurunda katika michezo yake miwili ya kutafuta tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Angola na zile za Kombe la Dunia zitakazofanyika Afrika Kusini mwaka 2010.

Stars, katika michezo yake hiyo imejikuta ikiambulia pointi moja baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Mauritius katika mchezo uliochezwa jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja Mpya wa Taifa, ambapo pia ilikubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa Cape Verde katika mchezo wa ugenini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashabiki hao walisema kuwa muda aliokaa Maximo na timu hiyo unatosha, ambapo kama ni kukibadili kikosi angeweza kufanya hivyo kama wanavyofanya makocha wengine.

Frank Magoba, mdau mkubwa wa soka hapa nchini alisema kuwa pamoja na Maximo kudai kuwa amekuza soka la Tanzania lakini ukweli utabaki pale pale kuwa hakuna alichokifanya na zaidi katika timu hiyo, ambapo alichokifanya yeye ni kuiweka Stars karibu na Serikali kwa kuwa ndiyo inayomlipa.

“Uwezo wa Maximo umefika mwisho hana jipya, haiwezekani tukawa tunafungwa na vitimu vidogo, halafu bado anajisifu amebadili mfumo wa soka letu, alichofanya yeye ni kuiweka Stars na TFF karibu na Serikali,“alisema Magoba.

Naye Nurdin Ezekieli alisema kuwa kwa matokeo haya tuliyoyapata ni ndoto kwa Stars kwenda Angola na hata Afrika Kusini kwa kuwa tulitakiwa kushinda katika mechi zote mbili kama walivyofanya Cameroon.

“Maximo bomu hawezi kutupeleka popote zaidi atazidi kuwatia Watanzania hasira kwa sababu ni ndoto kwa sisi kucheza fainali za Kombe la Dunia na hata zile za Mataifa ya Afrika,“alisema Ezekiel.

Kwa upande wake mchezaji wa zamani wa Stars, Thomas Kipese alisema kuwa wachezaji wa Stars hawajui wanachokifanya uwanjani na hilo linasababishwa na kocha kukosa ubunifu pale anapoona sehemu imepwaya.

“Kocha anatakiwa kuwa na maamuzi ya haraka, kama umeona mchezaji mpira umemkataa au nafasi flani uwanjani imepwaya unatakiwa kufanya mabadiliko, lakini hilo halifanyiki na zaidi wachezaji wetu hawajui wafanye nini pale linapojitokeza tatizo kama hilo,“alisema Kipese.

Stars itakuwa na kibarua kigumu cha kurudisha matumaini ya Watanzania juu yao hasa ukizingatia kuwa michezo yote iliyosalia ni migumu, ambapo Jumamosi itacheza na Cameroon hapa nchini na baadaye kurudiana nao nchini kwao kabla ya kurudi tena nchini na kupambana na Cape Verde.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments