Cameroon kuleta kikosi kamili

CAMEROON inakuja na kikosi chake kamili chenye wachezaji wote nyota wanaosakata soka Ulaya, akiwemo mshambuliaji nyota Samuel Eto’o na ndugu wawili, Rigobert na Alexander Song katika jitahada zake za kutotaka kurudia makosa ya mwaka 2005.

Cameroon, ambayo inaongoza Kundi la Kwanza la michuano ya awali ya Kombe la Dunia baada ya kushinda mechi zake mbili dhidi ya Cape Verde na Mauritius, inaonekana kupania kukata tiketi mapema baada ya kukosa fainali za mwaka 2006 zilizofanyika Ujerumani.

Katika kudhihirisha kuwa imepania, itawasili nchini siku nne kabla ya mechi hiyo, tayari kuivaa Stars Juni 14 kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), Frederick Mwakalebela alisema Comeroon inawasili leo, ikiwa na msafara wa watu 30, wakiwa ni viongozi 18 na wachezaji 20.

Mbali na Eto’o na akina Song, yumo kiungo wa zamani wa Chelsea, Njitap Geremi (Portsmouth), kiungo Stephene Etoub Mbia, ambaye aling’ara kwenye fainali za Mataifa ya Afrika, Modeste Mbami, na winga wa kulia aliyeichachafya Misri katika fainali nchini Ghana, Joel Diedonne Epale.

Kikosi kamili cha timu hiyo ni Esame Guy Stephen, Njitap Fotso Geremie Sorele, Alexandre Bilong Song, Sadjo Haman, Binya Augustin Cilles, Rigobert Bihanang Song, Bebbe Mbangue Custave Anicet, Kamen Idriss Carlos, Suleymanoun Hamidou na Atouba Essama Thimothee.

Wengine ni Bikey Amougou Andre Stephane, Mbia Etoub Stephen,Webo Kouama, Pierre Achille Nkong, Alain Mosely, Ngambi Alexis, Mbami Modester, Makoun Jean na Epale Joel Diendonne, Emana Endzimba Achille na Eto’o Fils.

Kikosi hicho kipo chini ya kocha wa zamani wa Senegal, Otto Pfister.

Wakati huo huo nahodha wa Stars, Henry Joseph ataukosa mchezo huo kutokana na kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwenye mchezo dhidi ya Cape Verde, ambao Stars ililala kwa bao 1-0.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments