Stars rojo kwa Cape Verde

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, jana usiku iliendelea kuwa `rojo` katika mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika 2010, baada ya kufungwa 1-0 ugenini na Cape Verde.

Huu ni mchezo wa pili wa Stars katika kinyang`anyiro hicho, ambapo katika mchezo wa kwanza timu hiyo ilitoka sare na wachovu Mauritius, katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa taifa wa kisasa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa TBC, bao hilo pekee katika mchezo huo lilipatikana katika dakika ya 72 na liliwekwa kimiani na Elvis Machido baada ya Edwardo kupiga mpira mrefu ulioshindwa kuzuiwa na Salum Sued na kumkuta Ivo Mapunda aliyejaribu kuokoa kabla hajamfikia mfungaji aliyeubetua kwa juu na kujaa wavuni.

Kwa matokeo hayo, Stars sasa imeshapoteza pointi tano na ina pointi moja tu mkononi, huku Jumamosi ikikabiliwa na kibarua kigumu wakati itakapocheza na Cameroon katika mchezo mwingine utakaofanyika jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha Stars kilikuwa;Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Salum Sued, Nadir Haroub `Canavaro`, Henry Joseph, Amir Maftaha, Godfrey Bonny, Athumani Idd/Kigi Makassy, Emmanuel Gabriel, Danny Mrwanda na Nizar Khalfan/Ulimboka Mwakingwe.

Katika dakika za mwisho, mabeki wa Stars ndio iliwabidi kufanya mashambulizi baada ya mbele kuoza, kwa mujibu wa mtangazaji wa TBC.

Matokeo mengine;Katika mechi za Kundi la 2, Kenya iliichakaza Guinea mabao 2-0, huku katika Kundi la 4, Afrika Kusini, Bafana Bafana, iliikandamiza Guinea ya Equator kwa mabao 4-1 wakati Tunisia iliitoa nishai Shelisheli kwa kuikandika mabao 2-0, katika mchezo wa Kundi la 9.

Katika mechi zingine juzi Ijumaa; Algeria iliifunga Liberia 3-0, katika mchezo wa Kundi la 3 wakati katika Kundi la 12, mabingwa wa Afrika Misri waliendelea kutoa onyo baada ya kuifunga Djibouti 4-0.

  • SOURCE: Lete Raha

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments