Yanga hatarini kufutwa uanachama-TFF

KLABU ya Yanga ipo hatarini kufutiwa uanachama wake katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na kutowasilisha katiba yao ili iendane na ya shirikisho hilo.

Klabu hiyo ni miongoni mwa vyama ambavyo havijawasilisha katiba yao na iwapo haitafanya hivyo hadi Juni 27 itafutiwa uwanachama wake.

Ofisa habari wa TFF, Florian Kaijage alisema juzi kuwa mkutano mkuu wa TFF uliofanyika Machi 29-30 uliazimia mabadiliko ya katiba za wanachama wa TFF.

Alisema maazimio hayo yalikuwa yanatakiwa yafanyike ndani ya siku 90 na siku hizo zinakamilika Juni 27 mwaka huu na kama kutakuwa na wanachama watakuwa hawajakamilisha basi wanafutwa uanachama wa TFF.

“Hadi Juni 27 chama ambacho kinajua ni mwanachama wa TFF kama hakijakamilisha usajili wake kitafutiwa uanachama,”alisema Kaijage.

“Muda tumetoa wa kutoa mapendekezo hayo, utekelezaji umekuwa ni wa taratibu mno, sasa tusije tukalaumiana kwenye hili itakapofika tarehe hiyo,”alisema.

Hadi jana, wanachama waliokuwa wamekabidhi katiba zao TFF ni Singida, Kagera, Rukwa, Mara, Lindi, Mbeya, Tanga, Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara, Arusha na vyama vilivyowakilisha ni Chama cha Madaktari wa Michezo (Tasma), na Chama cha Waamuzi (Frat).

Timu zilizoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambazo zimekwishawasilisha rasimu zao za katiba ni pamoja na Pan Afrika, Polisi Moro, Simba, Prisons na Manyema.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega alisema: ”Katiba haitengenezwi na TFF, inatengenezwa na wanachama, na sisi mkutano mkuu wetu tumepanga kuufanya Agosti 31 na moja ya ajenda katika mkutano huo ni kupitisha katiba.”

”Kwa mazingira hayo, itabidi tuwaombe TFF watupe muda, wao wanapendekeza mwisho wa kuwasilisha katiba, lakini sisi viongozi sio tunaotengeneza katiba ni wanachama na hii si kwa mujibu wa katiba ya Yanga tu bali ni vyama vyote,” alisema.

Timu ya Yanga uwanjani

TFF iliviagiza vyama wanachama wake kubadili katiba zao ili ziendane na za shirikisho hilo ikiwa ni pamoja na lile la kimataifa, Fifa na Afrika, Caf na moja katika baadhi ya vipengele ambavyo vinatakiwa kubadilishwa ni kile cha kuwa na katibu mkuu wa kuajiriwa badala ya kuchaguliwa.

Pia, ni marufuku masuala ya michezo kupelekwa mahakamani na badala yake ziundwe kamati ndogo ndogo zitakazosimamia.

Source:Mwananchi

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments