Euro 2008- na Mtazamo Wangu

Imeandikwa; na Israel Saria.

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1984, hakuna timu ya Taifa ya Uingereza katika mashindano haya makubwa katika bara la ulaya, hapa tunazungumzia Scotland, Ireland ya kaskazini na Wales.

Kwa ujumla wao haya mataifa yanaunda nchi inayoitwa Great Britain.

Kwa kushindwa kufuzu katika mashindano haya, hakuna kisingizio chochote kinachoweza kutolewa kukidhi haja ya mashabiki wa soka wa Uingereza. Kwa hiyo hakuna gwaride la Wake na Wasichana wa wanakandanda matajiri wa Uingereza (WAGs), pia hakuna hotuba za ’We can Win it’ kutoka kwa wanahabari na viongozi wasiokubali kushindwa bila kutoa sababu za msingi nchini Uingereza.

Pamoja na hali hiyo kutokea, hii haina maana kuwa wewe mpenzi wa soka, utaacha kukaa mbele ya runinga yako na kuwaangalia baadhi ya wanasoka nyota wanao tamba katika ligi kuu ya Uingereza.

Ufuatao ni uchambuzi wangu na kwanini uangalie Euro 2008.

CZECH REPUBLIC:Jamuhuri ya cheki

Sababu za kuishangilia hii timu ni pamoja na mfungaji wao Jan Koller, anayeongoza kwa ufungaji wa magoli, akiwa na magoli 52 katika mechi 83, anategemea kustaafu mara baada ya michuano hii ya Euro 2008. Katika michezo ya kimataifa ya mpira wa miguu, Koller ni mchezaji pekee anayemuangalia kwa chini Peter Crouch, jamaa kenda juu si mchezo. Wamefuzu kwenye michuano hii kwa ulaini, walianza vizuri na wakamaliza vizuri wana nafasi nzuri ya kufanya vizuri.

Wachezaji wanaocheza uingereza: Millan Baros (Portsmouth), Peter Cech (Chelsea), Marek Matejovsky (Reading).

PORTUGAL:Ureno

Sababu za kuishangilia hii timu, kwa upande wangu ni hizi zifuatazo: Mchezaji wa kiungo anayewika na ambaye kiwango chake cha uchezaji kiko juu sana kwa sasa, huyu ni Christiano Ronaldo, anavutia na amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Manchester United kwa msimu wa pili mfulizo katika ligi kuu na kombe la mabingwa wa ulaya hivi karibuni. Kocha wa timu hii ni Mbrazil Luiz Scolari au ‘Big Phil’ huyu kocha ni mshindi wa kombe la Dunia akiwa na timu ya kwao Brazil. Kwa vyovyote vile ni kocha mwenye jina kubwa na ambaye si mgeni miongoni mwa vyombo vya habari vya Uingereza kwani huko nyuma aliwahi kuhusishwa na Timu ya Taifa ya Uingereza.

Wachezaji wanaocheza katika Ligi kuu ya Uingereza: Jose Bosingwa, Ricardo Carvalho, Paulo Ferreira (Chelsea), Nani, Christiano Ronaldo (Manchester United).

SWITZERLAND:USWIZI

Sababu za kuishangilia hii timu ukiacha uzuri na umaarufu wa Nchi hii ambayo ni makao makuu ya Dunia ya Taifa lisilo na upande wowote (world capital of neutrality), ni idadi kubwa na yenye matumaini ya wachezaji wake wanaocheza nje.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Philipp Degan (Liverpool), Johan Djourou, Phillipe Senderos, ( Arsenal) , Brerim Dzemaili (Bolton), Gerson Fernandes (Manchester City)

TURKEY:UTURUKI

Sababu za msingi za kuishangilia hii timu, kwa hakika itakuwa sawa na kuiangalia Brazil kwani mchezaji wao wa kiungo Mehmet Aurelio au kwa jina maarufu ‘Marco Aurelio Brito dos PRAZERES’, ni moto wa kuotea mbali, huyu ni kiungo wa timu ya Fenerbahce.

Pia ni matumaini yangu kuwa mwalimu wa hii timu Fatih Terim, atatetea uamuzi wake wa kuacha kumwita kwene timu mchezaji mwenye ushawishi mkubwa Hakan Sukur.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Emre (Newcastle), na Tuncay Sanli (Middlesborough)

AUSTRIA:

Sababu za kufuatilia hii timu ni hizi zifuatazo: Ushiriki wao katika haya mashindano umefanya moja kati ya timu bora zaidi katika kutafuta timu zitakazo shiriki katika fainali hizi Scotland, kukosa nafasi kwa kigezo cha kuwa moja kati ya Nchi mwenyeji wa mashindano haya. Na pia ikumbukwe mchezo wao wa kirafiki na Uingereza ulitoa matokeo ambayo yaliwafanya Waingereza wajione kama mashujaa wasio na bahati, kumbuka Kuumia kwa Michael Owen, Kuitwa na kuachwa kwa David Beckam, na hali ya baadaye na hatimae kufutwa kazi kwa Kocha wa Uingereza.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Emanuel Pogatez (Middlesbrough).

CROATIA:

Nina kila sababu za kuihusudu hii timu, kwanza iliisambaratisha Timu ya Taifa ya Uingereza chini ya Steve McClaren, na hata Waingereza wanakubali kuwa Croatia wanastahili kuwa hapo walipo.

Walipoteza kwa Timu inayopewa nafasi nzuri ya kufanya vizuri katika mashindano haya, kwa kifupi ni kuwa Uingereza ilipoteza nafasi kwa mabingwa!.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Vedran Corluka (Manchester City), Luka Modric (Spurs), Niko Kranjar (Portsmouth).

GERMANY;UJERUMANI

Sababu zangu za kuamini ujerumani itafanya vizuri ni:

Mashindano ya kombe la dunia 2006, yanatukumbusha nini maana ya kuwa mjerumani nyumbani na ugenini, wajerumani wamekuwa na kasumba ya kujiona ni washindani halisi, linapokuja suala la mashindano makubwa, na bila shaka kuna ukweli ndani yake. Meneja wao wa zamani Jurgen Krismann, amekataa kuwa meneja wa timu ya Chelsea mara mbili nahii inaonyesha ni kwa kiasi gani kiwango cha mpira kilivyokua katika Ujerumani.

Wachezaji wa Ujerumani katika Uingereza: Michael Ballack (Chelsea)

POLAND;

Niionavyo Poland: Msafiri kafiri, ndivyo ninavyomuona mwalimu wa hii timu, kipenzi cha Cigar na mstaarabu fulani, huyu ni Leo Beenhakker, kocha mburudishaji hata kama wachezaji wake wamenuna. Uingereza inaweza kutofurahia mafanikio ya timu hii katika mashindano haya kwa sababu za kiuchumi zaidi, endapo Poland itasonga mbele katika mashindano haya, basi sekta muhimu zinaweza kujikuta hazina wafanyakazi, ukitilia maanani hawa jamaa wapo katika sekta muhimu katika maisha ya kila siku hapa Uingereza, japo katika unywaji ni watumiaji wazuri sana.

Wachezaji wanaocheza katika Uingereza: Tomasz Kuszcak (Manchester United) na Lukasz Fabianski (Arsenal)

FRANCE;UFARANSA

Nani atapingana na ukweli kuwa, nchi hii imepata mafanikio makubwa katika soka kutokana na sera zake za michezo, mara nyingi ukiiangalia ufaransa ikicheza utafikiri ni timu moja toka Afrika.

Ni mkusanyiko bora wa vipaji vingi visivyoisha kwenye chungu kikubwa cha hazina ya ufaransa na makoloni yake, sijui waingereza walikuwa wapi kuwekeza katika soka kwa makoloni yake? Tanzania, Kenya, Uganda, tungekuwa mbali sana kisoka kama hali kama hii ingekuwepo pia kwetu.Endapo Ufaransa itashinda mashindano haya, basi timu itakayo jisikia ni ‘mabingwa halisi’ itakuwa ni Scotland, kwani iliwafunga wafaransa mara mbili katika mechi za kufuzu katika mashindano haya.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Nicolas Anelka, Claude Makelele, Frorent Malouda (Chelsea), Lassana Diarra (Portsmounth), Partice Evra(Manchester United) na William Gallas (Arsenal).

HOLLAND;UHOLANZI

Niionavyo Holland: Wachezaji wa mjini hawa, wanatandaza kandanda safi kupindukia pia wanameremeta uwanjani na jina lao ni kama rangi ya chungwa inayofanana na jezi zao.

Mara ya mwisho kufanya kweli ni mwaka 1988, wanajiona kama timu isiyo na bahati, mara nyingi wanafanya vizuri mashindanoni ila hawashindi mashindano, kama vile Arsenal!.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Dirk Kuyt (Liverpool), Wilfred Bouma (Aston Vila), Mario Melchiot (Wigan), Andre Ooijer (Blackburn) ,Edwin van der Sar (Manchester United), Robin van Persie (Arsenal).

ITALY;ITALIA

Kwa maoni yangu hawa jamaa nawaona kama hivi: Ushindi wao wa kombe la Dunia mwaka 2006 ulikuwa wa kustahili hi ni kufuatia mchezo mzuri walioonyesha dhidi ya Ufaransa, bila kusahau kadi nyekundu kwa Zizo, katika mazingira ya kutatanisha, ilichangia kutoa matokeo ya mchezo huu mapema zaidi. Kashfa za kupanga matokeo katika ligi ya Utaliano, hili limetia doa mafanikio yao ya uwanjani, ghasia za mashabiki zilizopelekea mshabiki mmoja kupoteza maisha, mtazamo wa mpira wa nyumbani zaidi, ni Nchi kubwa na yenye mafanikio katika soka, laajabu ni haba sana kuona wachezaji wa utaliano wanacheza ligi za nje. Wametwaa kombe la dunia mara tatu, mara ya kwanza bila ya kuwa na mchezaji hata mmoja anayecheza soka nje ya utaliano.

Hata Marco Materazzi, ana wasiwasi juu ya hili.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Hakuna, ila Mwalimu wa England ni Mtaliano.

ROMANIA

Sababu za kufikiri watafika mbali ni hizi: Ni timu iliyotayari kufa uwanjani kwa ajili ya mafanikio ya nchi yao, na kuna uwezekano mkubwa wakaishia kwenye kundi la kifo, hapa watahitaji kila aina ya msaada toka miongoni mwao. Mwalimu wao Victor Pitura, alikuwa ni mchezaji wa Steaua Bucharest na alishiriki katika ushindi wa mikwaju ya penati mwaka 1986 iliyopelekea Bucharest kushinda kombe la Ulaya mwaka huo.

Wachezaji katika Uingereza: Hakuna, zaidi ya hawa ambao unaweza kusema walipitia tu na kwenda nchi nyingine, nao ni: Florin Raducioiu na Ilie Dumitrescu.

GREECE;UGIRIKI

Sababu kubwa ya kuipenda hii timu, ni pale walipomfanya Christiano Ronaldo alie uwanjani pale waliposhinda kombe hili nchini Ureno Mwaka 2004.

Hii timu inawashangaza wengi kwa aina ya mchezo wao, miguvu, kukimbia sana uwanjani na kucheza bila tabasamu uwanjani.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Hakuna.

RUSSIA;URUSI

Nionavyo hii timu:

Hii timu inasaidiwa kwa kiasi kikubwa na Roman Abromovich, kwa mazamo wangu ataendelea kupoteza umaarufu mpirani kwa kutumia pesa nyingi kutafuta mafanikio.

Kwa kupoteza kwa Manchester United katika fainali kule Moscow, naamini hakuna cha kutumainiwa, ni aibu kuona walitumia nyasi bandia uwanjani kuwafunga waingereza katika michuano ya kufuzu, huku waingereza wakienda Luton, kujizoeza jinsi ya kucheza kwenye nyasi bandia, huku mtaalamu wa uwanja wa hizo nyasi bandia ni mwingereza, japo hapa Uingereza hakuna kiwanja hata kimoja kinachotumika kwa mashindano chenye nyasi bandia.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Hakuna, ila kila timu inatamani sana kumpata mchezaji mwenye kipaji wa kiungo Andrea Arshavin.

SPAIN;HISPANIA

Kwa Mtazamo wangu, hawa jamaa wana rekodi mbaya zaidi kuliko Uingereza katika michuano mikubwa ya Ulaya na Dunia, ila ni timu ya kuangaliwa kwa umakini sana, wana ari ila haionekani.

Ligi yao ni kubwa na maarufu, na ni ligi yakistaarabu kulinganisha na ligi nyingine zenye kashfa na migogoro, ni Ligi inayowekwa pamoja na Ligi ya Uingereza kwa kuwa na majina makubwa ya wachezaji na ni ligi yenye pesa nyingi.

Wachezaji wanocheza Uingereza: Xabi Alonzo, Alvaro Arbeloa, Jose Reina, Fernando Torres (Liverpool), Cesc Fabregas (Arsenal).

SWEDEN;

Naingalia vipi hii timu ? Kwangu mimi ni aina ya wachezaji walioko ndani ya kikosi hiki. Nina uhakika kabisa hii itakuwa ni mara ya mwisho kuwaona wachezaji kama Henrik Larsson, mara baada ya kutangaza kustaafu na kubadili mawazo zaidi ya mara tatu, bila shaka hii itakuwa ni ‘Final Hurrah’ kwa michezo ya kimataifa kwa nyota huyu aliyewahi kuwika na vilabu kama Celtic, Barcelona, Man utd nk. Larsson akishirikiana na Zlatan Ibrahimovic bila kumsahau Freddie Ljungberg kwa pembeni bila shaka itakuwa ni burudani zaidi, kuliko mchezo wenyewe.

Wachezaji wanaocheza Uingereza: Andreas Granqvist (Wigan) ,Andreas Isaksson (Man City), Sebastian Larsson (Birmingham), Freddie Ljungberg (West Ham).

Comments