Viingilio Vya Mechi Ya Taifa Stars Na Cameroon Vyatajwa

SHIRIKISHO la Soka Tanzania limetangaza kiingilio kikubwa kwa ajili ya mechi baina ya Tanzania na Cameroon itakayofanyika Juni 13 jijini Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia, kiingilio cha juu kikiwa ni Sh50,000.

Mechi hiyo, ambayo pia inatumika kama michuano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Angola mwaka 2010, itachezwa jijini Dar es Salaam Juni 14.

Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage alivitaja viingilio vingine kuwa ni Sh 40,000 kwa VIP B, Sh20,000 kwa VIP C.

Pia alisema kiingilio kwa jukwaa lenye viti vya rangi ya machungwa vinavyotazamana na Jukwaa Kuu ni Sh20,000, wakati viti vya rangi ya machungwa vya nyuma ya magoli ni Sh 10,000 viti vya bluu mzunguko Sh7,000 na Sh5,000 kwa viti vya kijani.

Kaijage alisema tiketi hizo zitaanza kuuzwa Jumatatu au Jumanne ijayo na kwamba TFF imeamua kutangaza viingilio mapema kutokana ma umuhimu wa mechi yenyewe.

Wakati huo huo, Kaijage alisema Stars itaondoka nchini keshokutwa saa 11 alfajiri kwenda Praia, nchini Cape Verde kucheza mechi yake ya pili ya michuano hiyo ya Dunia na Afrika baada ya kulazimishwa kwenda sare ya bao 1-1 nyumbani na Mauritius katika mechi ya kwanza.

Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Morocco wakati kamisaa ni N’diaye Birame kutoka Senegal.

Mechi hiyo itachezwa Jumamosi Saa 10.00 kwa saa za Cape Verde ambazo ni sawa na saa 12.00 za jioni kwa upande wa Tanzania.

Aidha, Kaijage alisema mashabiki ambao wangependa kwenda huko kuishangilia timu hiyo wanatakiwa kulipa dola 1,000 badala dola 1,225 zilizotangazwa awali.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments