Serikali yamtetea Marcio maximo

SERIKALI imesema kuwa suala la kuongezwa au kutoongezwa kwa mkataba wa kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo halina budi kuachwa kwa sasa kwa kuwa kulizungumzia ni kama uchuro.

Mkataba wa miaka miwili wa kocha huyo Mbrazili unamalizika Agosti na mashabiki wa soka, ambao walikuwa wanataka asiongezewe mkataba, sasa wamegawanyika baada ya Stars kuonyesha maendeleo makubwa katika mechi za hivi karibuni.

”Kwa nini tuzungumzie mkataba wa kocha wakati muda wa kumalizika kwake haujafika,” alisema Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera alipozungumza na Mwananchi jana.

”Kocha bado anafundisha, hatuna kocha mwingine na muda wa mkataba wake bado haujamalizika, kwa nini tuanze kuzungumzia… si itakuwa ni uchuro?”

”Nadhani suala la mkataba wake tuliache kwa sasa hadi hapo utakapomalizika. Si imebaki miezi michache, tuache kwanza. Tukizungumzia sasa tutakuwa kama tunaweka uchuro.”

”Na hata hivyo, kuna taratibu nyingi za kufuata baada ya kumalizika kwa mkataba wake. Itatubidi pia tupate maoni kutoka (Shirikisho la Soka) TFF kama wanaona ni mzuri na wakipenda aendelee, ataendelea na kama hawamtaki, ataondoka.”

Mashabiki wa soka walikosa uvumilivu kwa Mbrazili huyo, kutokana na Stars kushindwa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika Ghana mapema mwaka huu, lakini baada ya timu hiyo kuziondoa Kenya na Uganda katika michuano mipya ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) na kuonyesha soka safi katika mechi zilizoisha kwa sare dhidi ya Malawi na Mauritius, mashabiki sasa wanaona kuwa tatizo ni wachezaji.

Maximo, ambaye aliahidi kuanza kujenga ngome na baadaye kiungo kabla ya kujenga safu ya ushambuliaji, amepoteza mechi tano, ikiwemo moja ya Kombe la Chalenji alipoiongoza timu ya Bara, ameshinda mechi 10 na kutoka sare mechi 11.

Mashabiki pia wamekuwa wakimpinga kocha huyo kutokana na msimamo wake wa kutoita baadhi ya wachezaji kwenye timu yake, akiwemo kipa wa Simba, Juma Kaseja, ambaye alimtema mara baada ya timu kurejea kutoka Senegal, ambako Stars ilichapwa mabao 4-0.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments