China waanza sherehe hata kabla ya michezo kuanza


SALA, nyimbo, maandamano na sherehe za hapa na pale ziliutawala mji mwenyeji wa michezo ya Olimpiki mwaka huu, Beijing, Jumatano kusherehekea kubaki kwa siku 100 kabla ya kuanza kwa michezo hiyo huku wengi wakitumaini kuwa itakuwa ya mafanikio.

Tofauti na michezo iliyotangulia, maandalizi ya Beijing yamekwenda kama yalivyopangwa na tayari viwanja kadhaa na miundombinu vimekamilika.

Jiji hilo limetumia kati ya dola bilioni 35 hadi 40 kuboresha miundombinu kama vile viwanja vya ndege na barabara zake, pamoja na dola bilioni 2.1 kwa ajili ya kuendeshea michezo hiyo.

“Siku 100 baadaye zitaleta raha ya ajabu na furaha hapa Beijing. Wananchi na wageni wataliona jiji likijibadilisha wakati likiwapokea wanamichezo, waandishi wa habari na watazamaji kwa ajili ya michezo hii mikubwa,” alisema Ofisa wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC).

Lakini kwa miezi michache iliyopita maandalizi murua ya michezo hiyo yalikumbwa na simanzi wakati mwenge wa Olimpiki ulipokuwa ukipata upinzani mkubwa katika mbio zake sehemu kadhaa duniani huku waandamanaji wakihoji rekodi ya China kwenye haki za binadamu, hususan sera zake huko Tibet.

Sherehe za Jumatano zilifanyika chini ya wingu lenye ukungu na mbio za wakazi 10,000 wa Beijing kuzunguka eneo la kijani la Olimpiki (Olympic Green) kama ahadi ya China kuifanya michezo hiyo ya watu wote.

Upande mwingine, Kanisa Katoliki la China liliendesha ibada ya kuiombea mafanikio michezo hiyo. Mtawa mmoja mwanamke aliiambia Reuters kwamba wamewasamehe wote waliozichafua mbio za mwenge wa Olimpiki.

“Bila shaka tumesamehe vyote vilivyofanywa na watu wasiojua siasa,” Angela Teresa Ying alisema baada ya misa iliyofanyika kanisa kuu la Beijing kuombea michezo hiyo.

China imekwishasema haitasumbuliwa na maandamano hayo na imepanga kuandaa ‘Michezo ya Olimpiki ya Hali ya Juu’.

“Ingawa watu kadhaa wenye ajenda za siri wamejaribu kuiingilia na kuipakazia vibaya michezo hii…hii haitabadili nia ya Wachina bilioni 1.3 kuandaa michezo hii kwa ajili ya dunia nzima,” gazeti linalolisemea chama cha kikomonist, People’s Daily, lilisema katika tahariri yake.

Jiji hilo lipo tayari kuzuia kurudiwa kile kilichofanyika wakati wa kushereheke mwaka mmoja kabla ya michezo hiyo ambapo wanaharakati wa uhuru wa Tibet walipoupanda ukuta wa China (Great Wall) na kuchafua hali ya hewa ya Beijing na kusababisha mvua za ajabu zilizosimamisha shughuli zote jijini humo.

Usalama jijini Beijing imeonekana kuimarika zaidi kufuatia maandamano ya mwezi uliopita huko Tibet, mbio za mwenge wa Olimpiki na kauli ya China kwamba wameuvunja mpango wa magaidi wa kuvamia michezo hiyo.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments