Maximo Mtegoni Tena

Hali ya baadaye ya nafasi ya kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo iliwekwa shakani jana Jumamosi baada ya timu hiyo kutoka sare ya bao 1-1 na Mauritius kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, katika mechi ya ufunguzi ya Kundi la Kwanza la michuano ya awali ya Kombe la Dunia ambayo wenyeji walipata kona 19.

Bao la kusawazisha la Stars lilifungwa katika dakika ya 69 na Danny Mruanda anayecheza soka Kuwait. Baada ya mechi hiyo, Stars inakabiliwa na michezo mitatu mfululizo migumu na timu mbili zinazopewa nafasi kubwa kwenye Kundi la Kwanza, ikiwemo miwili ya ugenini na wa nyumbani dhidi ya Cameroon wiki mbili zijazo. Katika mchezo huo, Stars si tu ilipoteza nafasi nyingi, nyingi za kufunga ilizotengeneza, bali pia ilikosa penalti na kuwazawadia wageni goli kutokana na shambulio lao la kwanza. Mpira wa juu uliorudishwa kizembe na mlinzi Nadir Haroub `Canavaro` kwa mlinda mlango Ivo Mapunda uliwahiwa na mshambuliaji wa Mauritius Marquette Wasley katika dakika ya 39 na kumuacha na kazi nyepesi ya kumzunguka kipa huyo.

Katika mechi nane zilizotangulia baina ya timu hizo tangu mwaka 1968, Mauritius imeshinda mara tatu na jana ilielekea kuwa ni nafasi ya Stars kwenye kisahani cha dhahabu kusawazisha rekodi hiyo baada ya kuweka kambi kwenye lango la wageni kwa dakika 38 za kwanza. Emmanuel Gabriel alifunga kutokana na mpira wa kwanza wa penalti iliyotolewa na muamuzi Kenias Marenge kutoka Zimbabwe katika dakika ya 35 baada ya Henry Joseph kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari, lakini adhabu hiyo ilibidi irudiwe kutokana na mpira kupigwa kabla ya filimbi ya muamuzi.

Gabriel alipiga vilevile na mpira huo wa mara ya pili ambao ulidakwa na mlinda mlango wa Mauritius Amomothoo Francis. Lakini kama hali ilivyokuwa kabla ya bao la kusawazisha la Stars, na licha ya kutolewa nje kwa mfungaji wa wageni, wachezaji wa pembeni wa Stars walishindwa kupiga krosi zilizotolewa kuwa kona ambazo hazikuisadia timu ya taifa, na Maximo hakuonekana kuwa na uwezo wa kurekebisha kasoro hiyo. Maximo, aliwaomba radhi Watanzania kwa sare hiyo, lakini alijitetea kwa kusema tatizo la timu hiyo ni safu ya ushambuliaji, ambalo eti, ni kwa nchi nzima.

Mchezo wa pili wa Stars wa kundi hilo ni dhidi ya Cape Verde Jumamosi. Timu zilikuwa: Stars: Ivo Mapunda, Fred Mbuna, Amir Maftaha (Jerson Tegete dk.63), Salum Sued, Nadir Haroub `Canavaro`, Godfrey Bonny, Henry Joseph, Nizar Khalfan (Athuman Idd `Chuji` dk.87), Danny Mruanda, Emmanuel Gabriel (Kigi Makassy dk.66) na Ulimboka Mwakingwe.

* SOURCE: Lete Raha

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments