Taifa Stars yatoka sare nyumbani, yapoteza nafasi nyingi za wazi!!

PAMOJA na kupata nafasi nyingi za kufunga, Stars jana ilijikuta ikishindwa kuzitumia nafasi hizo na kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Mauritius katika kampeni zake za kwanza za kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika mwaka 2010.

Mauritius ndio ilianza kuziona nyavu za Stars dakika ya 39 ya mchezo kupitia mchezaji wake Wesley Marguette kutokana na uzembe wa Salum Sued, huku kipa Ivo Mapunda akiwa nje ya goli.

Stars ilisawazisha bao hilo dakika ya 64 kupitia kwa Danny Mrwanda akiwa amepokea pasi kutoka kwa Sued.

Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, Stars ilianza kwa kasi mchezo huo huku ikishambulia lango la Mauritus lakini ubutu wa safu ya umaliziaji ndio uliyoingusha Tanzania.

Taifa stars vs Mauritius

Kwa hesabu za haraka haraka Stars imepoteza kona zaidi ya 18 na penati moja kutokana na umaliziaji butu.

Sekunde ya 10 Stars ilipeleka shambuzi kali langoni mwa Mauritus, lakini ilijikuta ikipata kikwazo kutokana na ngome imara ya wapinzani hao.

Dakika moja Mrwanda alishindwa kutumia vema pasi ya Ulimboka Mwakingwe na kujikuta akikosa bao, dakika ya nne Henry Joseph alipeleka mashambulizi hayakuzaa matunda na kuambulia kona butu, huku Emmanuel Gabriel akipoteza mipira mingi ya wazi dakika ya nne alipata nafasi lakini alipaisha mpira juu.

Stars itajutia nafasi ilizopata hasa kipindi cha kwanza dakika ya 16 Henry Joseph aliachia shuti kali mita 20 lakini kipa wa Mauritius, Francois Ammomoothoo alipangua, na dakika ya 30 alikosa bao la wazi.

Dakika ya 35 mwamuzi Marange Kenias kutoka Zimbabwe alitoa penati kwa Stars baada ya Henry Joseph kufanyiwa madhambi eneo la hatari, lakini Emanuel Gabriel alikosa penati hiyo baada ya kipa wa Mauritus kuiona.

Awali Gabriel alipata penati hiyo lakini mwamuzi Kenias aliikataa na kuamuru ipingwe upya baada ya wachezaji wa Stars kuingia ndani ya penalti kabla ya filimbi kupulizwa.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo alisema “Kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wangu ni kizuri lakini hatujashinda, wametengeneza nafasi nyingi nzuri lakini mpira si hesabu, Mauritius nawapongeza kwa jinsi walivyofanya kazi nzuri ya kuzuia inagawa tumeonyesha kiwango kizuri na mashindanio ndio yaanaza sasa,”alisema Maximo.

”Mechi ya leo ilikuwa ni muhimu lakini tumetoka sare sina furaha na matokeo haya, nawapa hongera Mauritius kwa sababu ngome yao ni nzuri, timu imeonyesha kila kitu lakini tumeshindwa kushinda…..”

Siwezi kusema makosa ya mchezaji mmoja mmoja kama kupoteza timu imepoteza pamoja na kama kushinda timu inashinda pamoja mimi si aina ya makocha wanaoponda wachezaji mmoja mmoja, kiwango kilichoonyeshwa leo na timu yangu kinanipa matumaini,”alisema Mbrazili huyo.

Wakati Maximo akisema hayo, kocha wa Mauritius Chundunsing alisema “Nimefurahishwa na kiwango cha wachezaji wangu, wamecheza nilivyotaka, kwa mujibu wa maelekezo niliyowapa, tungefungwa mechi ya leo ingekuwa hatari sana kwangu kwa sababu ndio tumeanza mashindano, lakini huu ni mpira na mara nyingi unabadilika,”alisema kocha huyo ya Mauritus…..

Hata hivyo pamoja na ubora wa uwanja katika Afrika Mashariki, utaratibu uliotumika jana ulikuwa mbovu na uliosababisha usumbufu kwa baadhi ya washabiki na wengine kupigwa virungu.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida washabiki walikuwa wanaingia uwanjani hapo bila utaratibu maalum na hatimaye wale waliokuwa wanalipa viingilio vya sh 30,000 na 20,000 walijikuta wanakaa pamoja na wale waliolipa sh 3000 kutokana na utaratibu mbovu wa kuingilia uliotumika.

Hali hii ilikuja kuwa kero kubwa na kusababisha baadhi ya washabiki kupigwa virungu na askari waliokuwa wanalinda usalama uwanjani hapo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa washabiki waliokuwa wamelipa viigilio vya bei husika.

Washabiki wengine walikaa kwenye maeneo haya makusudi huku wengine wakikaa bila kujua kuwa wanachofanya ni kosa kutokana na kutopata maelekezo kutoka kwa wasimamizi.

Hali hii ilianza dakika 10 kabla mpira haujaanza baada ya kundi kubwa la washabiki waliokuwa wamelipa viingilio vya Sh 20,000 kukosa nafasi ya kukaa na hatimaye Afisa wa Habari wa Shirikisho la Soka, Florian Kaijage alikwenda na kuchukua askari watatu ambao walianza kukagua tiketi za watu waliokuwa wamekaa eneo hilo.

Zaidi ya asilimia 70 ya watu wote walikuwa wameketi eneo hilo walikuwa hawana tiketi husika na kusababisha usumbufu mkubwa.

Hata hiyo baadhi walifanya ubishi na hatimaye askari waliamua kutumia virungu kuwapelekea sehemu inayostahili.

Baada ya kuona nguvu vimetumika washabiki wengi walikimbia hivyo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wale ambao baadae ulijulikana kuwa ulisababishwa na wasimamizi wa nje ya uwanja ambao walionekana kuwa hawajui lolote kuhusu Uwanja huo na hatimaye kuwafaya washabiki waingie maeneo wanayotaka.

Wakati huo huo washabiki zaidi ya watatu jana walikamatwa na askari baada ya kuanza fujo ikiwa ni pamoja na kurusha chupa za maji.

Washabiki hao ambao wote walikuwa wa jinsia ya kiume walikubwa na dhahama hiyo muda mchache baada ya kipindi cha pili kuanza.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments