ZFA yavunja ndoa yake na TFF

Chama cha Soka cha Zanzibar, ZFA, kimevunja rasmi ndoa yake na Shirikisho la Soka nchini, TFF, baada ya kuona TFF haitekelezi makubaliano waliyoafikiana kwenye vikao vyao mbalimbali walivyokutana.

Kwa mujibu wa barua ya Rais wa ZFA, Ali Ferej Tamim aliyoituma kwa Rais wa TFF, Leodger Tenga na nakala kuzisambaza kwa Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Zanzibar na Bara na kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa MBT na lile la Zanzibar, imeonyesha kuwa ZFA wamekerwa na vitendo vinavyofanywa na TFF.

Katika barua hiyo ambayo inakichwa cha habari Dharau na ukiukwaji wa makubaliano ya Vikao kati ya ZFA na TFF,imeweka wazi masuala mbalimbali ambayo ZFA na TFF waliafikiana lakini yamekuwa kinyume.

Baadhi ya mambo yaliyokiukwa na TFF ni kukaa kimya ama kujiamulia wanapotaka wao vikao na ZFA, ambapo inakuwa ngumu pale ZFA inapohitaji kukutana na TFF kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali, ambapo vikwazo vingi vimekuwa vikijitokeza.

Tamim, alisema kuwa walikubaliana misaada inayotolewa na bodi ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA na lile la Afrika CAF, igawiwe na Zanzibar lakini suala hilo halijafanyika, pia walikubaliana Zanzibar kushiriki katika semina na mafunzo ya FIFA lakini cha kushangaza hata taarifa haipelekwi ZFA.

Mbali na hayo Tamim aliongeza kuwa TFF imekuwa ikikaa kimya na dola 250,000 zinazogawiwa na FIFA, lakini hakuna hata senti inayopelekwa huko pia uteuzi wa makocha wasaidizi kwenye timu za Taifa, hauzingatii ushirikiano na makubaliano yaliyofikiwa kwenye vikao, ambapo TFF imekuwa ikifanya inavyotaka.

Aidha, aliongeza kuwa TFF, imekuwa ikiyafuta majina ya waamuzi wa Zanzibar kwenye orodha ya majina ya waamuzi wanaohitajika kupewa beji za FIFA, ambapo pia TFF imepokea mradi wa Gold, kutoka FIFA, mara mbili mmoja ukiwa wa kujenga hosteli na mwingine wa kuweka nyasi bandia katika viwanja viwili.

Cha kushangaza miradi yote imeelekezwa bara badala ya angalau kuutupia mmoja Zanzibar.

ZFA, pia imelalamikia suala la kusafiri kwa timu ya taifa, Taifa Stars, ambapo kimsingi kunatakiwa kuwe na mwakilishi mmoja kutoka Zanzibar lakini hilo halifanyiki pamoja na kutumia fedha zote zinazotumwa na CAF ambazo ni dola 100,000.

Alisema kuwa kwa hali hiyo ZFA imechoshwa na imeamua kusitisha mahusiano na TFF hadi pale vyombo vya juu vya soka Duniani vitakapoliamua suala hilo, ambapo wanatarajia kuviandikia barua.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alisema kuwa suala hilo limekaa kisera zaidi, ambapo hawezi kuliongelea hadi pale Tenga atakapolitolea maamuzi.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments