Stars yakaribia fainali

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars jana Jumamosi ilipiga hatua kubwa kupata nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani baada ya kuitoa Uganda kwa jumla ya mabao 3-1 katika raundi ya pili ya awali.

Stars ambayo ilitoka sare na Uganda ya bao 1-1 hapa Kampala katika mchezo wa marudiano wa raundi ya pili uliofanyika kwenye Uwanja wa Nakivubo, itacheza na mshindi wa mchezo kati ya Rwanda na Sudan kuwania kucheza fainali za mwakani nchini Ivory Coast.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Sudan, wenyeji walishinda kwa magoli 4-0.

Lango la Stars jana lililindwa na kipa wake aliyekuwa amefungiwa kucheza soka kwa kipindi cha miezi sita kutokana na kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu na klabu yake ya Yanga, Ivo Mapunda.

Na ilikuwa ni bahati mbaya kwamba mchezaji huyo anayeaminiwa mno na kocha mkuu Marcio Maximo aliwajibika kwa bao la kwanza la mchezo, la Uganda, katika dakika ya saba baada ya kutema mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Dan Wagaluka na kuwahiwa na Godfrey Sserukuma aliyesukumiza wavuni.

Lakini Stars ilisawazisha katika dakika ya 44 kupitia kwa kiungo Athuman Idd `Chuji` aliyeunganisha mpira wa kona iliyochongwa na Amiri Maftaha.

Kuingia kwa chipukizi Jerson Tegete aliyechukua nafasi ya mkongwe Emmanuel Gabriel, Kigi Makassy akimbadili Ulimboka Mwakingwe na Uhuru Seleman akiingia badala ya `Chuji` kulifanya sura ya mchezo ibadilike kwa mashambulizi zaidi kuelekea langoni mwa wenyeji lakini mlango wa wenyeji ulikuwa mgumu.

Maximo alisema amefurahi timu yake imecheza kwa kujiamini, na matokeo yaliyotokea ndio aliyokuwa akiyahitaji, na sasa anaangalia zaidi mechi za michuano ya awali ya Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika ambapo Taifa Stars ipo kundi moja na Cameroon, Cape Verde na Mauritius.

Mipambano hiyo ya awali ya Kombe la Dunia itafanyika kati ya mwishoni mwa mwezi huu na wiki tatu za kwanza za Juni.

Kocha wa Uganda Laszlo Csaba raia wa Hungary alisema amekubaliana na matokeo kwani Stars walicheza vizuri, ila sasa nguvu anazielekeza kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Awali kabla ya mchezo msafara wa Tanzania uliokuwa na Stars, viongozi wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ulifanyiwa vurugu ya kuzuiwa kuingia uwanjani kwa madai ya malipo ya viingilio,.

Mohamed Nassor, mjumbe wa TFF kutoka Kigoma alilipa dola 200 za Marekani na msafara kuruhusiwa kuingia uwanjani.

Katibu wa TFF Frederick Mwakalebela alisema wamewasilisha barua ya malalamiko kwa kamisaa wa mchezo huo kutokana na vurugu hizo, pia kunyimwa uwanja wa kufanyia mazoezi baada ya timu hiyo kuwasili nchini Uganda.

Timu zilikuwa:
Stars: Ivo Mapunda, Fred Mbuna, Amir Maftaha, Nadir Haroub `Canavaro`, Salum Sued, Godfrey Bonny, Shabaan Nditi, Athuman Idd (Uhuru Seleman dk. 85), Emmanuel Gabriel (Jerson Tegete dk. 60), Mrisho Ngassa na Ulimboka Mwakingwe (Kigi Makassy dk.61).

Uganda: Hamza Muwonge, Julius Mulindwa, Steven Senoga, Mussa Doka, Joseph Owino, Johnson Bagoole, dan wagaluka, Steven Bengo (Robert Ssentongo dk.46), Geofrey Ssrukuma, Caesar Okuti (Owen Kasule dk.46) na Antony Bongole.

  • SOURCE: Lete Raha

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments