Rais Kikwete na Timu ya Taifa ya soka

RAIS Jakaya Kikwete, ambaye anajulikana kuwa mpenzi mkubwa wa soka, hapendi timu ya taifa, Taifa Stars ipoteze mechi nyumbani, wachezaji wa Stars wamedokezwa.

Ufunuo huo uliwekwa bayana juzi usiku wakati Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika alipozungumza katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuwapongeza wachezaji wa Taifa Stars kwa kuishindi Uganda kwa mabao 2-0 iliyofanyika kwenye hoteli ya New Africa.

“Tena nimekuja kuwaambieni Rais Kikwete hataki timu ishindwe nyumbani,” alisema Mkuchika kabla ya kukabidhi Dola 100 za Kimarekani kwa kila mchezaji kama pongezi kwa ushindi huo.

Mkuchika hakufafanua zaidi kauli hiyo, lakini akasema kuwa walikuwa wakisubiri kwa hamu kuona hilo linatekelezwa wakati wakati Stars ilipoikaribisha Uganda kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jumamosi iliyopita.

“Kazi bado,” alisema Mkuchika, ambaye ni kepteni mstaafu wa jeshi.

“Wakati mkiongoza kwa mabao 2-0, tulikuwa tunaomba bao la tatu lije ili kazi iwe ngumu kwa Waganda nyumbani kwao. Lakini haikuwezekana, hivyo mnapoenda kwao, msiende kujihami. Ongezeni goli, halafu mengine yafuate.”

Rais Kikwete alikuwepo katika mechi ya kwanza ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali zilizopita za Mataifa ya Afrika wakati Taifa Stars ilipoikaribisha Burkina Faso kwenye Uwanja wa Taifa.

Katika mechi hiyo, Stars ilishinda kwa mabao 2-1, lakini akakosa mechi ya mwisho baina ya Stars na Msumbiji kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, wakati wageni waliposhinda kwa bao 1-0. Alikosa mechi hiyo kwa kuwa alikuwa na shughuli za kikazi mkoani Arusha, lakini aliongea na wachezaji siku moja kabla ya mchezo huo.

Stars haikuweza kufuzu baada ya kushindwa kulinda uongozi wake wa bao 1-0 dhidi ya Senegal mjini Mwanza na baadaye kuruhusu kipigo hicho cha nyumbani. Katika mechi nyingine za michuano hiyo, Stars ilitandikwa mabao 4-0 na Senegal jijini Dakar, ikatoka suluhu na Msumbiji jijini Maputo na kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Burkina Faso jijini Ouagadougou.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments