Waamuzi wachezeshe kwa haki kombe la Taifa!!

KOMBE la taifa limepangwa kuanza kutimua vumbi Jumanne ijayo kwa kushirikisha timu 23 kutoka mikao yote ya Tanzania bara.

Shindano hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania, TBL kupitia bia yake ya safari.

TFF na TBL, walisaini mkataba wa Shilingi bilioni 1.54 wa kudhamini mashindano kwa miaka mitatu, Sh milioni 580 zikitumika kila mwaka kuanzia mwaka huu ambao mashindano hayo yataanza rasmi kesho kwa Iringa kumenyana na Manyara kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Asilimia 90 ya maandalizi ya mashindano hayo kwa upande wa wadhamini na TFF yamekamilika kwa njia moja ama nyingine.

Ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa TBL iliendesha semina kwa waandishi wa habari za michezo iliyofanyika Jumamatano iliyopita kwenye ukumbi wa hoteli ya Wet n Warld jijjini Dar es Salaam.

Moja ya ajenda kubwa ambayo ilizua mjadala mkubwa ni juu ya waamuzi wabovu ambao wamekuwa wakitoa maamuzi tata ama kwa makusudi kutokana na mapenzi yao kwa timu fulani ama kwa kutofahamu vizuri sheria za soka.

TFF imekuwa ikitoa semina mbali mbali kabla na baada ya ligi ili waamuzi kujua majukumu yao kabla ya mashindano husika kuanza.

Nia ya semina hizo kwa waamuzi ni kuwakumbusha wanaochezesha mechi wachezeshe kwa haki pasipo malamiko yoyote na kufuata sheria zote za mchezo wa soka.

Tumeona kasoro nyingi zilizojitokeza katika ligi iliyomalizika hivi karibuni kwa Yanga kutwaa ubingwa na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya klabu bingwa Afrika.

Tumesikia malalamiko mengi kwa waamuzi sababu iliyofanya TFF kuchukua hatua kali ikiwa ni kuwafungia baadhi ya waamuzi waliovurunda katika mechi zao walizochezesha na hata wengine kushushwa daraja la uamuzi.

Mjadala ulioibuka kwa waandishi wa habari ni kutaka TFF ichukue hatua kali zaidi kwa waamuzi watakaoboronga kwenye mashindano ya Kombe la Taifa kwa kuwa wamekuwa wakiziumiza timu na kuacha makovu kwa timu iliyoonewa, na adhabu zinazochukuliwa zimekuwa hazitoshi ndio maana wimbi la waamuzi wabovu limekuwa likiibuka siku hadi siku.

Hili liko wazi na linaeleweka kwamba waamuzi wanachezesha wanavyojua wao. Sunday Kayuni aliyekuwa mkufunzi wakatika semina hiyo alikiri waamuzi wabovu ndio wanaorudisha nyuma soka la Tanzania.

Hatuamini licha ya kuwa TFF ilitangaza kuhakikisha waamuzi wanaochezesha mashindano hayo wana ubora wa ngazi ya Fifa na daraja la kwanza.

Ni ukweli usiopinginga waamuzi wamekuwa kichocheo kikubwa cha vurugu uwanjani kwa kutoa maamuzi yasiyofaa kutokana na sababu zao binafsi.

Mashindano haya ya Kombe la Taifa yanaendeshwa kwa njia ya mtoano, iwapo mwamuzi atatoa maamuzi mabovu ni wazi atakuwa anaiumiza timu husika na kuacha kovu kubwa lisilofutika.

Kimsingi waamuzi wajue wana jukumu kubwa mbele yao, na semina wanazopewa na TFF za mara kwa mara waonyeshe kuwa zinatoa manufaa na kuleta mabadiliko uwanjani kwa kufuata sheria 17 za soka na kuweka mbali ushabiki na unazi kwenye soka.

Waamuzi tunajua kuwa ndio wasemaji wa Mwisho uwanjani, maamuzi yao yanaweza kuwa faida au hasara kwa timu fulani iwapo hawatazingatia miiko ya fani yao na kutoa maamuzi ya ajabu ajabu.

Tusingependa kuona mashindano ya Kombe la taifa yanaharibika kwa sababu ya ubovu wa mtu mmoja au kikundi cha watu fulani.

Tunataka kuona ushindani wa kweli, na sio ubabaishaji na kubebana pasipokuwa na msingi, tunapenda kuona timu zenye ubora ndio zinazosonga mbele kwenye mashindano hayo badala ya kufanyiwa mizengwe na kutolewa kwenye mashindano hayo kwa mizengwe isiyokuwa na msingi.

Mashindano hayo yatatoa dira na mwanga kwa mikoa husika ambayo baadhi yao imekuwa hazina timu za ligi kuu na ni changamoto kubwa kwa mikoa kuhakikisha wanaziendeleza timu hizo hata kama zitatolewa kwenye mashindano na kuhakikisha siku zinapanda kucheza ligi kuu.

Mkoa kama wa Kigoma ni mkoa ambao ulisifika kwa soka sana miaka ya nyuma, hakuna staa wa soka ambaye chimbuko lake halikuanzia Kigoma, lakini mkoa huo hivi sasa upo duni kisoka.

Mkoa kama Kilimanjaro, Tabora, Singida na mingine mingi haipo kabisa kwenye ramani ya soka kutokana na kukosa timu zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara.

Sitaki kuamini kama mikoa ambayo haina timu za ligi kuu zimekosa wachezaji, sitaki kuamini kuwa kwenye mikoa hiyo hakuna wachezaji ambao wana kiwango cha hali ya juu ambao wangeweza kuonekana na kuitwa kwenye timu za taifa.

Tunataka Kombe la taifa lirudi kama miaka ya nyuma, lilete msisimko kama siku za nyuma wachezaji wa timu za taifa walipatikana kutokana na mashindano ta Kombe hili la taifa.

Miaka ya nyuma kuna wachezaji ambao hawakuwai kuchezea timu kubwa lakini walikuwa ni wachezaji mahiri wa kutumaini kwenye kikosi cha timu ya taifa.

Mchezaji kama Hamis Gaga aliyekuwa akicheza timu ya Ndovu Arusha na baadaye Simba wakati huko ikiwa daraja la pili Arusha, alikuwa ni namba nane ya kudumu ya timu ya taifa na hiyo yote alionekana kupitia kombe hili la taifa.

Ni wazi Watanzania sasa wanataka mabadiliko kwenye medali ya soka, waamuzi, wadau wabadilike, washikamane na kuhakikisha msisimko hule wa miaka ya 80 unarudi.

Tunataka Kocha wa timu ya taifa ya vijana, Marcus Tinoco na yule wa Taifa Stars, Marcio Maximo, wafike mahali wachague wachezaji kutoka madaraja ya chini na kuachana na wakongwe wa Ligi Kuu na hiyo yote itawezekana kama mashindano hayo ya Kombe la taifa yatahamasishwa na kupewa msukumo mkubwa ambayo utaibuka vipaji vya vijana chipukizi katika medali hii ya soka.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments