Tanzania yaibuka kidedea mbele ya Waganda kwenye soka

TANZANIA Taifa Stars Jumamosi iliwapa watanzania raha tena baada ya kufanikiwa kuichapa timu ya Taifa ya Uganda “The Cranes” mabao 2-0 kwenye mchezo mkali wakutafuta tiketi ya kucheza michuano ya mabingwa wa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Stars baada ya wiki chache zilizopita kufanikiwa kuitupa nje timu ya Taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 2-1 huku Uganda ikifanikiwa kuitoa Elitrea kwa jumla ya mabao 3-0.

Stars ikiwa na kikosi kile kile kilichoitoa Kenya isipokuwa kiungo Geofrey Bonny alichukua nafasi ya Athumani Idd aliyekuwa na kadi mbili za njano, ilianza mchezo wa jana kwa makeke makali na katika dakika ya 3 walikuwa wameshapiga hodi langoni mwa Uganda baada ya Uhuru Suleimani kupiga krosi lakini shuti la Amir Maftah likaokolewa na mabeki wa Uganda.

Bao la kwanza la Stars liliwekwa kimiani na Emanuel Gabriel katika dakika ya 12 baada ya kupata krosi safi toka kwa mshambuliaji machachari Mrisho Ngassa na kuunganisha mpira kimiani.

Shaabani Ndity aliyeingia kuchukua nafasi ya Henry Joseph mwanzoni mwa kipindi cha pili aliipatia Stars bao la pili katika dakika ya 60 baada ya kona safi iliyopigwa na Amir Maftah na kumkuta Nadil Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alipiga kichwa kilichopanguliwa na kipa wa Uganda na kumkuta Nditi aliyepiga shuti kali na kutinga wavuni.

Katika dakika ya 15 Laurence Segawa alipewa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Mrisho Ngassa ambaye alikuwa akiisumbua ngome ya Uganda kila mara.

Kipindi cha kwanza Stars walionyesha kiwango cha hali ya juu na kulisakama lango la Uganda muda mwingi wa mchezo.

Kipindi cha pili Stars walifanya mabadiliko baada ya Henry Joseph kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Shaaban Nditi, Uhuru Suleiman alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Ulimboka Mwakingwe Uganda alitoka Jeremiah Sebuyira na nafasi yake kuchukuliwa na Jonhson Bangole.

Dakika za mwanzo katika kipindi cha pili Uganda walitawala mchezo lakini Stars walitumia mwanya huo kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Katika dakika ya 63 Uganda walikosa bao baada ya kipa wa Stars Farouk Ramadhan kuupangua mpira ambao uliwahiwa na Nadil Haroub aliyeonyesha uwezo wa hali ya juu jana.

Stars itapambana na Uganda wiki mbili zijanzo nchini Uganda na endapo itafanikiwa kuwatoa Waganda basi itakuwa imebakiza dakika tisini za mchezo kati yake dhidi ya Sudan au Rwanda na mshindi kati hapo atafuzu kwenda kwenye Fainali hizi zitakzofanyika kwa mara ya kwanza nchini Ivory Coast.

Kocha Msaidizi wa Stars Ally Bushir alisema Stars imefanikiwa kupata ushindi kutokana na kuungwa mkono vizuri na washabiki wa mkoa wa Mwanza pamoja na kutumia vizuri nafasi walizopata.

Huku Kocha wa Uganda Gsaba akisema timu yake imecheza mchezo mzuri kuliko Stars lakini wameshinda kuweka mpira kimiani ingawa anaamini kuwa watafanikiwa kuitoa Stars katika mchezo wa pili utakaofanyika nchini Uganda wiki mbili zijazo.

Kikosi cha Stars jana kilikuwa Farouk Ramadhani,Fred Mbuna ,Amir Maftah Nadil Haroub Cannvaro,Salum Swed Geofrey Bonny, Henry Joseph/Shaaban Nditi, Abdi Kassim Emanuel Gabriel/ Jerry Tegete , Mrisho Ngassa, na Uhuru Suleimani/ Ulimboka Mwakingwe.

Uganda iliwakilishwa na Sam Kawalya Simon Masaba, Laurence Ssegawa, Musa Doka, Joseph Owino,Owen Kasule, Daniel Wagaluka, Stephen Bengo Geofrey Serunkuma, Gaesar Okuthi na

Jeremiah Sebuyire.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments