TFF yakiri katiba ya vyama vingi vya soka zimepitwa na wakati

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limekiri katiba nyingi za vyama vya soka zina kasoro ndiyo maana vimekuwa vikifanya kazi kibabaishaji.

Hayo yalisemwa juzi kwenye semina elekezi ya waandishi wa habari iliyofanyika Kunduchi nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya Michuano ya Kombe la Taifa.

Wakichangia mada mbali mbali zilizowasilishwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF Sunday Kayuni na rais wa Shirikisho hilo Leodegar Tenga waandishi wa habari walitaka kujua inakuwaje baadhi ya wajumbe wanaowakilisha mikoa kwenye kamati za TFF wanaishi Dar es Salaam huku mikoa yao ikiwa duni kisoka.

”Kuna wajumbe utakuta anadai anawakilisha Kigoma na kaingia TFF kwa mgongo wa Kigoma lakini makazi yake na shuguli zake zote zipo Dar es Salaam huko Kigoma anasaidieje kwa maendeleo ya soka?”

Akijibu swali hilo, Kayuni alisema: ”Ni kazi kubwa kubadilisha akili za watu waachane na mambo ya mwaka 47 na kuwa na usasa,” alisema Kayuni ambaye pia ni kocha mzoefu.

Katiba zina kasoro nyingi, hao watu wa Kigoma na kwingineko ndio wanatakiwa kulipigia kelele na kutolifumbia macho suala hilo, ni kweli mkoa kama Kigoma ndio uliokuwa unasifika kwa soka, asilimia kubwa ya wachezaji maarufu hapa nchini wametokea Kigoma lakini leo hii Kigoma hakuna hata timu ya Ligi Kuu, Kigoma imekufa kabisa kisoka.

”Mwenyekiti na Katibu wanasikia raha kuitwa mwenyekiti wa klabu fulani, wapo kwa maslahi yao binafsi wanajiingia kwenye uongozi ili kupata chaneli za biashara zao, hakuna malengo kabisa.”

Naye rais wa TFF Leodegar Tenga alisema kutokana na matatizo hayo ya ubovu wa katiba na viongozi kujali maslahi yao binafsi badala ya klabu wanazozitumikia ndio waliochangia kulifikisha soka la Tanzania hapa lilipo sasa.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments