Mchezaji chipukizi huenda akauzwa ulaya

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga na Taifa Stars, Jerryson Tegete ni mmoja wa wachezaji waliotajwa kutakiwa kwenda kufanya majaribio ya soka nchini Norway.

Wakala wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), (Tanzania) Meddy Rhemtullah alisema jana kuwa wachezaji watatu ambao anatarajia kuwapeleka nje kwa ajili ya majaribio ya soka yumo Tegete, lakini hajafikia maafikiano na mchezaji huyo.

Mpaka sasa sijajibiwa barua yangu na viongozi wa Yanga kuomba niruhusiwe kumpeleka Tegete kwenye majaribio barani Ulaya, alisema.

Alisema wachezaji wengine ambao ameshaongea nao na kuwaombea ruhusa katika klabu zao ni Caeser Okuti wa Uganda na Yaneitla Guiton wa Eritrea.

Alisema kwa upande wa wachezaji aliowapeleka mwaka jana ni mmoja ndiye ameonekana kufanya vizuri, Suleiman Ndikumana wa Burundi ambaye anachezea timu ya Molde FK iliyoko Norway ambayo ameingia mkataba wa miaka mitatu.

Alisema kuwa mkataba wake unamfanya alipwe Shilingi 6 milioni kwa mwezi na akicheza mechi au akivaa jezi na kukaa benchi kama mchezaji wa akiba anakuwa akilipwa posho ya si chini ya Shilingi milioni moja.

Alisema kwa upande wa Uhuru Suleiman alishindwa kufanya vizuri, lakini kocha wa timu aliyokuwa anafanya majaribio hayo alisema kuwa ni mchezaji mzuri na atakuwa mchezaji mzuri, ingawa anakosa baadhi ya vitu muhimu.

Alisema kocha huyo alisema atamuita tena kwa ajili ya majaribio ya pili kama siyo timu yake atamtafutia timu nyingine ya kufanyia majaribio.

Katika hatua nyingine, Rhemtullah alisema viongozi wawili kutoka timu ya Molde FK ya Norway ambao ni mkurugenzi wa klabu, Tarje Jackobsen na kocha msaidizi Tare Hagh wamewasili jana kwa ajili ya kuanzisha shule ya michezo Tanzania.

Alisema viongozi hao watatembelea shule zote za mchezo wa soka zilizoko Dar es Salaam, watazungumza na viongozi wa klabu zilizopo kwenye ligi na viongozi wa Shirikisho la Soka la Tanzania, TFF na wakifikia muafaka watasaini mkataba wa ujenzi wa shule hiyo.

Aliongeza kuwa shule hiyo itakuwa kila mwaka inatoa wachezaji wawili kwenda kucheza nje ya nchi na wachezaji wengine watakuwa wanauzwa katika timu za nje ili kuinua soka nchini.

Comments