Yanga kutwaa ubingwa leo?

Ikiwa inahitaji pointi mbili na kuweza kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam kucheza na JKT Ruvu.

Awali mechi hiyo ilitarajiwa kufanyika jana, lakini kutokana na tukio la kukimbizwa kwa mwenge wa Olimpiki ilisogezwa mbele kwa siku moja.

Endapo Yanga itashinda mechi hiyo leo itakuwa imefikisha pointi 49 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo hatazikishinda mechi zake zote zilizosalia.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa Yanga itacheza kufa na kupona ili kuondoka na ushindi na kucheza mechi zilizosalia kwa kutimiza ratiba tu.

Ina nafasi nzuri kutokana na kukabiliana na JKT Ruvu kutokuwa katika nafasi ya kushuka daraja au kushika nafasi za juu za ligi hiyo.

Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa vita kubwa iko katika kuwania kushiriki katika mashindano ya Kombe la Shirikisho kati ya timu za Prisons ya Mbeya na Simba.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwenye uwanja huo kwa kuwakutanisha Bingwa watetezi, Simba na Toto Africans kutoka jijini Mwanza kwenye uwanja wa Taifa.

Simba ambayo iko katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 34 ilipoteza matumaini ya kulichukua taji hilo tena baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Moro United Jumatano iliyopita kwenye uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.

Ligi hiyo mwaka huu inadhaminiwa na Vodacom na kituo cha televisheni cha kulipia cha GTV.

Wakati huo huo, Samson Barnabas anaripoti kutoka Mbeya kuwa Prisons iliiichapa Moro United katika mechi ya Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyochezwa katika uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kwa matokeo hayo sasa imefikisha pointi 41 na kuizidi Simba pointi saba na kujiweka katika nafasi nzuri ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani.

  • SOURCE: Nipashe

Comments