Hatimaye Taifa Stars Yashinda

TIMU ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ jana ilifanya kile kilichokuwa kinasubiliwa kwa muda mrefu na mashabiki wengi wa soka baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Harambee Stars.

Taifa Stars jana iliuanza mchezo huo kwa taratibu huku washambuliaji wake wakipoteza nafasi nyingi za kufunga katika kipindi cha kwanza.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Marcio Maximo katika kipindi cha pili ya kumtoa Fred Mbuna na kumwingiza Jerryson Tegete yalikuwa na faida kubwa kwa timu hiyo.

Mshambuliaji Jerryson Tegete ndiye aliyekuwa wa kwanza kupachika bao kwa Taifa Stars na kurudisha matumaini kwa mashabiki wachache waliokuwa wamehudhuria mchezo huo kipindi cha pili.

Baada ya bao hilo Stars waliongeza mashambulizi langoni mwa Harambee Stars na katika dakika ya 93 beki Nadir Haroub ‘Canavaro’ alipata bao la pili baada ya piga nikupige langoni mwa Harambee Stars kutokana na mpira wa kona iliyopigwa na Kiggi Makasi.

Kwa matokeo hayo sasa Taifa Stars imefuzu kwa hatua ya pili ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) na sasa itakutana Uganda ambayo imefuzu kwa hatua hiyo baada ya kuifunga Eritrea kwa jumla ya mabao 5-1.

Ushindi huo wa leo umerudisha hari ya watanzania kuonyesha mapenzi yao kwa timu yao ya taifa ambayo yalipungua kufutia timu hiyo kufanya vibaya katika mechi kadhaa za hivi karibuni.

Harambee iliingia uwanjani ikilinda goli lao moja waliofunga nyumbani kwao wiki mbili zilizopita huku muda mwingi wakitumia kujiangusha uwanjani.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo Kocha wa timu ya taifa Marcio Maximo ambaye muda mwingi kipindi cha kwanza alionekana kuwa na presha zaidi alisema “Presha pati ya mpira kama hutaki presha kaa ofisini, naandaa timu hivi sasa kwa ajili ya Uganda kwani ipo juu sana kwenye Fifa ranking kutuzidi sisi, mchezo utakuwa mgumu kwetu,”alisema Maximo ambaye alishangilia kwa nguvu sana lilipoingia bao la pili na kuingia uwanjani kukumbatiana na wachezaji wake.

“Ndio maana nasema nipewe muda na wachezaji wapewe muda tunaitaji maandalizi mazuri ili tuweze kufuzu mashindano yetu,”alisema Maximo.

Naye Kocha wa Harambee Stars Jacob ‘Ghost’ Mulee ambaye alishikwa na butwaa kuona timu yake ikiondolewa kwenye mashindano alisema “Naipa ongera sana Stars wamefanya bidii kwenye mechi hasa kipindi cha pili wametupa presha kutufunga,”alisema Mulee kwa uzuni kubwa uku mikono ikiwa shavuni.

Katika mchezo huo wa jana viongozi wawili wa TFF nusura wamvae mwandishi wa Televisheni ya taifa (TBC) kwa madai ya kuponda wachezaji wa timu ya taifa.

Viongozi hao wawili Msafiri Mgoyi na Danny Msangi walimvurumushia matusi mwandishi huyo ambaye dakika karibu zote za mchezo alikuwa akiponda wachezaji wa Stars kuwa hawana lolote.

Comments