Wanafunzi wafanya Vizuri katika Michezo Dar..

WANAFUNZI wa Taasisi ya Tanzania Sports Academy (TSA), ambayo inamiliki shule ya Sekondari ya Wining Spirit ya jijini Arusha, jana waling’ara katika mashindano ya Dar Coca Cola Half Marathon yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Katika mashindano hayo ya kilomita 21, wanariadha kutoka mikoa mbalimbali walionekana kuzidiwa nguvu na washiriki kutoka Arusha walioshinda nafasi za juu.

Katika mbio hizo zilizoanza majira ya saa 12:00 asubuhi zikifunguliwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Nkaya Bendera, washindi 10 bora kwa upande wa wanaume walitoka mkoani Arusha huku kwa upande wa wanawake nafasi tano zilichukuliwa pia na wanariadha kutoka mkoa huo.

Mbio hizo zilizidisha ladha zaidi baada ya wakimbiaji mahiri kushindwa kufua dafu dhidi ya chipukizi walioonyesha vipaji vyao, ambako kwa upande wa wanawake bingwa wa Kilimanuaro Marathon, Banuelia Brighton alishindwa kuonyesha makeke yake baada ya kushika nafasi ya sita.

Hali hiyo ya washindi wengi kupatikana kutoka Arusha ilimstua hata mgeni rasmi katika mashindano hayo, Bendera na kutaka wakazi wa Dar es Salaam kufanya mazoezi ya nguvu zaidi, ikiwezekana kuwe na timu bora ya riadha.

Hata hivyo, Bendera aliishukuru Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yameonyesha ari, baada ya watu wengi kujitokeza kushiriki mbio za kilomita 21 na zile za kilomita 5 za kujifurahisha ambako hata baadhi ya watoto walishiriki.

Aliongeza kuwa Coca Cola isiache utaratibu wa kuandaa mashindano hayo kila mwaka, hata kama hakuna tukio kubwa linalokuja kama la mbio za Mwenge wa Olimpiki bali wafanye kila mwaka ili kuweza kuvumbua vipaji vilivyojificha.

Washindi watano wa kwanza katika mbio za kilometa 5 walikabidhiwa zawadi zao na Waziri Bendera huku nafasi ya sita hadi ya kumi walikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro ambako mshindi wa kwanza hadi wa tatu walizawadiwa zawadi za medali.

Mshindi katika mashindano ya kilometa 21 kwa upande wa wanawake, aliibuka Janeth John Yuda ambaye ni mke wa mwanariadha mahiri wa John Yuda kutoka TSA, ambaye alitumia saa 1:15.05 na kujinyakulia kitita cha sh milioni moja, huku nafasi ya pili ikienda kwa Sara Ramadhani kutoka Zanzibar aliyetumia muda wa saa 1:15.06 akipata sh 750,000 huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Mary Noel pia kutoka Arusha aliyetumia saa 1:17.55 na kuondoka na sh 500,000.

Mshindi wa nne upande wa wanawake aliibuka Fabiola William ambaye ni mshindi wa Kilimanjaro Marathon 2008, aliyejinyakulia sh 300,000, huku wa tano akiibuka Frola Charles wa Arusha aliyepata sh 250,000, huku anayeshikilia rekodi ya taifa ya marathon kilometa 42 ambaye pia ni mshindi wa Kilimajaro Marathon 2008, Banuelia Brighton kutoka Moshi akishika nafasi ya sita na kujinyakulia sh 200,000, na kufuatiwa na Jackline Sakila kutoka Zanzibar sh 150,000, Tausi Said kutoka Arusha sh 100,000, Sara Majah kutoka CCP Moshi sh 750,000 na Zaituni Jumanne wa Arusha sh 50,000.

Kwa upande wa wanaume, nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Marco Joseph ambaye ni mwanafunzi wa Sekondari ya Wining Spirit ambayo inajihusisha na kuendeleza vipaji vya wanariadha aliyetumia saa 1:03.24, nafasi ya pili ikichukuliwa na Rogart John Akhwari aliyetumia saa 1:03.31 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Peter Sulle saa 1:03.32.

Waliofuatia nafasi ya nne hadi ya kumi na zawadi zao kwenye mabano ni Faustine Mussa (300,000), Samwel Shauri (250,000), Samson Ramadhani ambaye ni mwanamichezo bora wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) 2007, na mshindi wa medali ya dhahabu katika mashindano ya Jumuiya ya Madola akijinyakulia sh 200,000, aliyefuatiwa na Pascal Mombo wa klabu ya African Ambasador Athletic Club (AAAF), Sh 150,000, Daniel Chopa ambaye ni mshindi wa Kilimanjaro Air Tanzania Nusu Marathon sh 100,000, na mshindi wa pili Kili Marathon 2008, Andrea Silvine sh 750,000 huku Anold Masai akifunga kumi bora na kujinyakulia sh 500,000.

Kwa upande wake Meneja Masoko Mwandamizi wa Coca Cola Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Caroline Mbaga alisema kuwa, wamepokea ushauri uliotolewa na Waziri Bendera na kuahidi kuufanyia kazi na kuwataka Watanzania wajiandae kwa mashindano mengine kama hayo hapo mwakani.

Mashindano hayo maalumu yaliandaliwa na Coca Cola ambao ni kati ya wadhamini watatu wa michezo ya Olimpiki, ikiwa ni shamrashamra za kuukaribisha mwenge wa Olimpiki unaotarajiwa kukimbizwa jijini Dar es Salaam Aprili 13 likiwa ni jiji pekee barani Afrika.

Kwa upande wa kilometa tano, wanafunzi wa Sekondari ya St Patrick ya Madale jijini Dar es Salaam walitawala ambako Mohammed Idd akishika nafasi ya kwanza na kufuatiwa na Ingo Ranko Banadi huku nafasi ya nne ikienda kwa Mgosi Otengo, na Vicent Rono akishika nafasi ya 22.

Kwa upande wa wanawake, Angelina John alishika nafasi ya pili, Maria Shinje nafasi ya tatu, Agnessy Luwanja ambaye anaibukia kwa kasi katika fani ya riadha akishika tano.

Kwa upande wa kilometa 21, pia St Patrick haikulala baada ya Tabu Mwandu kushika nafasi ya 39 huku kwa wanaume, mlemavu Wilbert Costatine akishika nafasi ya 38 na Richard Petro 23.

Wadhamini wengine wa michezo ya Olimpiki ni kampuni ya vifaa vya umeme ya Samsung na kampuni ya kompyuta ya Lenova.

Mbio hizo pia zilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo akiwamo mbunge wa zamani wa Kilolo, Venance Mwamoto, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, Kanali Juma Ikangaa, Filbert Bayi na wengineo.

Comments