Simba yakung`utwa 7-1

Simba yakung`utwa 7-1 2008-04-07 09:22:49 By Somoe Ng’itu Pamoja na Simba kuwatilia ngumu wapiga picha wa televisheni, wawakilishi hao wa Tanzania jana waliungana na watani zao Yanga kukaa kando ya mashindano ya kimataifa baada ya kufungwa na Enyimba ya Nigeria kwa mabao 3-1, katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa. Simba imeondolewa katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa jumla ya mabao 7-1 kufuatia kupokea kipigo cha 4-0 Aba, Nigeria katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili wa mashindano hayo. Wenzao Yanga juzi Jumamosi walishindwa kufurukuta baada ya kupokea kipigo cha 1-0 nyumbani kutoka kwa timu ya Libya Al Akhdar na kufungasha virago katika mashindano ya Shirikisho kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kutoka 1-1 ugenini wiki mbili zilizopita. Simba ilionekana kama ingeweza kuibuka na ushindi mnono baada ya kupata bao katika dakika ya tano tu ya mchezo kupitia kwa Athumani Machupa akiunganisha wavuni krosi safi ya Ramadhani Wasso. Hata hivyo, Enyimba walitulia na kusawazisha kupitia kwa Steven Worgu aliyefunga kirahisi baada ya mabeki wa Simba kuzumbaa na kutoa mwanya kwa mfungaji kuujaza mpira wavuni katika dakika ya 14. Enyimba ilifunga bao la pili katika dakika ya 19 kupitia kwa Jasaih Maduabuchi baada ya kumshinda mbio Victor costa, aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu. Wageni Enyimba walijipatia bao la tatu dakika moja tangu kuanza kwa kipindi cha kwanza kwa bao lililofungwa na Uche Kalu baada ya kumtoka beki mahiri wa Simba Ramadhan Wasso. Julius Mrope na Machupa walikosa mabao katika dakika ya 70 na 73 licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini walichemka. Simba ilipata pigo katika dakika ya 87 baada ya mchezaji wake Juma Nyoso kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumvuta jezi mshambuliaji wa Enyimba Falodin Omaseun. Katika hali isiyokuwa ya kawaida wachezaji wa Simba walitumia chumba cha kubadilishia nguo cha Yanga huku viongozi wao nao wakikaa upande wa wapinzani wao hao, kitu ambacho hakijawahi kutokea. Uongozi wa Simba ulitangaza mapema kuwa hautaruhusu kabisa wapiga picha wa televisheni, kwani hakuna kituo kilichowafuata kutaka kuonyesha mchezo huo. Hata hivyo, Simba waliwazuia hata wale walikuwa wakitaka kuchukua picha kwa ajili ya habari tu. Timu zilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Nico Nyagawa, Ramadhan Wasso, Nurdin Bakari/Juma Nyoso (dk.68), Victor Costa, Mohamed Banka, Moses Odhiambo, Mussa Hassan Mgosi/Joseph Kaniki (dk.46), Athumani Machupa, Emmanuel Gabriel/Julius Mrope (dk.62) na Ulimboka Mwakingwe. Enyimba:Sani Hariri, Ajibade Omolade, Okeng Emigozo, Peter Ebibor, Okey Odita, Oga Okqara, Jasalih Maduabuach, Stephen Worgu, Uche Kalu, Dady Bazuaye na John Oweri. * SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  , ,

Comments