Mpaka lini tutaendelea kuwa kichekesho kwenye Michezo!!

Kwanza nitoe pole kwa wachezaji wote wa timu ya Taifa, timu ya Simba na timu ya Yanga pale walikofikia kwenye michezo ya kimataifa. Naandika haya kwa masikitiko makubwa sana. Tumerudi nyuma sana katika swala la michezo.


Sababu zinazotufanya tusionekane kwa muda mrefu na kufanya vizuri kwenye michezo ya kimataifa ni hizi zifuatazo.
Tuanze na Vilabu.
1. Vilabu vyote vya mpira Tanzania vinachukuwa wachezaji wenye kujisifu,kujiona,kutojiamini, na wasiojituma.
2. Wachezaji wanacheza mpira bila malengo. Hawajui kuwa mpira wa miguu ni pesa na umeshatajirisha wachezaji wengi sana duniani.
Wanapoingia kucheza na timu za nje ya nchi wanasahau kuwa kuna vyombo vingi sana vinawaangalia. Wanapaswa wawe na juhudi binafsi kama sio juhudi za kufunzwa ili kujiuza katika soka duniani.
3.Elimu ya wachezaji waliowengi sio nzuri sana ukilinganisha na wachezaji wa Africa Magharibi. Kuna haja ya kuwa na waalimu wa lugha katika vilabu kusudi wachezaji wajifunze lugha waweze kuelewa hasa makocha. Kuanzishwe somo la lugha hasa kingereza.
4. Wachezaji wanakuwa na ubinafsi wakiwepo uwanjani. Hawaweki malengo na taratibu nani atayarishwe kwa ajili ya kutafuta magoli na nani atayarishwe kwa ajili ya kufunga magoli.
5. Hawajui kuwa mpira unapokuwa golini kwao ni madhara kwa timu yao. Hivyo wafundishwe jinsi gani ya kuuondoa kwenye eneo lao mipira isiyo ya lazima. Wapunguze milundikana hasa mwenzao anapokuwa anamiliki mpira.
6. Hawafanyi mazoezi ya kutosha kuongeza pumzi ya kuwepo uwanjani kwa mda mrefu. Pia mlo wanaokula sio wa kuimarisha afya zao. Kuwepo mda wa kujifunza ni mlo gani unafaa kwa mchezo wa mpira na mlo gani unafaa kwa mtu anayecheza mchezo wa kuogelea.
MUHIMU:
La muhimu katika yote wafundisheni wachezaji wa vilabu na timu ya taifa kuwa mpira wa miguu ni kazi kama kazi zingine na ndio maana watu kama Droba waliacha kuwa madaktari na kukimbilia mprira. Sasa hivi ni matajiri sana. Waufanye mchezo wa mpira wa miguu kuwa ni ajira na wajue kuchezea klabu ni mwanzo wa kujulikana. Waache Maringo wawapo uwanjani. Ringa ukishapata mafanikio sio uringe wakati ndio uko kwenye darasa la mpira wa miguu. Jenga nia kuwa umeshaona nchi fulani hivyo lazima ushinde mechi uone nchi nyingine. Wingi wa timu zetu zinaishia mechi za awali kwa kuwa wachezaji kwa pamoja hawaweki mikakati ya kuongeza jiografia yao. Umeona Nigeria au Libya weka nadhiri ya kuona Congo, Angola,Misiri, nk.
TIMU YA TAIFA
Mimi naamini kwa asilimia mia moja Dar es salaam hakuna wachezaji wanaoweza kuunda timu ya taifa. Tuunde timu ya Taifa kutokana na timu za mikoa. Nasema kuwa timu za mikoa pia zinakuwa na wachezaji kutoka vilabu mbalimbali. Hii itasaidia kujenga morali kwa kila mchezaji kwa kuwa atajua kuwa akilemaa tu ameachwa. Kocha wa timu ya taifa ashirikishwe kuangalia mechi za kombe la taifa la mikoa yote Tanzania kusudi kusiwepo upendeleo wa kuchagua wachezaji wa kuunda timu ya taifa. Tofauti na sasa hivi mchezaji wa Simba, Yanga,Mtibwa anajiona ni yeye tu atachukuliwa kumbe kule mikoani kuna vijeba vya mpira. Nenda Tanga,Mwanza,Arusha,Kigoma,Morogoro,Shinyanga, Mtwara, nakuambia ukishindanisha hii mikoa hakuna mchezaji wa Simba na Yanga atapata namba labda yule aliyestuka mapema kuwa janja ya Walimu ni kukutanisha watu kuchuja viwango.
Mwisho tunapochezea katika uwanja wa nyumbani iwe ni timu ya taifa au vilabu tuache kucheza mchezo wa kufungwa kwanza ndio tuanze kutafuta magoli ya kusawazisha. Timu zetu zimekuwa na tabia hizo. Kwa nini sisi kama Taifa Stars au Mtibwa au Simba au Yanga tusianze kwanza kufunga mabao kujipunguzia mzigo wa kusawazisha mabao?.


Bao la kusawazisha siku zote ni bao gumu sana kufunga kwani tayari umeshaathika kisaikolojia kuliko goli la kumtangulia adui kufunga kwani hili linakupa faraja, na nguvu ya kuongeza lingine.Turudisheni heshima za wachezaji wetu wa zamani kina Sembuli,Mambosasa,Kibaneni,Sunday Manara,Kitwana Manara,Tenga,Willy Mwaijibe, Abdalah Hussein, Chogo, Abas Dilunga,Maulid Dulunga, Chuma na wengineo.
Mwanamichezo mwenzenu mstaafu.
Richard Reward Kilonzo
Arusha – Tanzania

Comments