Simba Ina Kibarua Kigumu Kwa Enyimba

SIKU moja kabla ya Simba kuvaana na Enyimba katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa, klabu hiyo imelalamikia tatizo la majeruhi kuwa linaweza kuiathiri kesho, huku mashabiki wa timu hiyo ya Nigeria wakitabiri kipigo kingine kikubwa.

Mabeki wa kati, Kelvin Yondani na Henry Joseph wana kadi zinazowazuia kucheza mechi hiyo, wakati beki mzoefu, Victor Costa, Nassoro Said, Chollo, na Said Sued bado hawajawa fiti kukabiliana na Enyimba, ambao wameshatwaa ubingwa wa Afrika mara mbili.

Hali hiyo inafanya mabingwa hao wa soka nchini kusaliwa na Juma Said ,Nyoso na Deogratius Naftari, ambao hawana uzoefu wa kucheza kati, lakini angalau itakuwa na uhakika pembeni ambako Nurdin Bakari na Ramadhan Wasso watakuwepo.

�Sued na Chollo wanatuchanganya sana kwa kuwa uwezekano wa kucheza kwao ni mdogo wakati ni wachezaji tegemeo, alisema meneja wa Simba, Amri Said ‘Stam’.

Sued anasumbuliwa na nyonga mara kwa mara wakati Chollo bado hajapona mguu hivyo kuna uwezekano mdogo kwao kucheza.Makao makuu ya Club ya Simba, Msimbazi

Hata hivyo, Amri alijipa moyo kuwa ingawa wachezaji hao ni muhimu katika mechi hiyo ngumu, lakini wapo wengine wanaoweza kuziba mapengo hayo.

Katika hatua, Enyimba International ya Aba, wamefungua nafasi (zone) kwenye tovuti yake kutoa nafasi kwa mashabiki kubashiri matokeo ya mechi ya Jumapili na Wanigeria wengi wanaona mabingwa hao wa zamani wa Afrika wataibuka na ushindi wa kuanzia mabao mawili jijini Dar es salaam.

Simba ilifungwa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza mjini Aba wiki mbili zilizopita na inahitaji miujiza ya mwaka 1978 kushinda kwa mabao 5-0 Jumapili ili iweze kusonga mbele, lakini mashabiki waliotuma ujumbe kwenye tovuti hiyo wanaona hilo halitawezekana.

Enyimba, ambayo ilikuwa klabu ya kwanza ya Nigeria kutwaa ubingwa wa Afrika, imefungua sehemu hiyo kwenye tovuti yake ili kuwapa mashabiki hao nafasi ya kubashiri matokeo ya mechi hiyo na nyingine.

“Tumewapa nyinyi kitu kipya cha Prediction Zone (Nafasi ya Ubashiri). Mechi ya Simba na Enyimba nchini Tanzania inakuja katika muda chini ya wiki moja na tunataka kujua mnafikiria nini kuhusu matokeo ya mechi hiyo muhimu ya Ligi ya Mabingwa,” anasema mhariri wa tovuti hiyo.

Katika maoni hayo wengi wanaona kuwa Enyimba inaweza kushinda hata kwa mabao 4-1.

“Simba 1 Enyimba 4. Enyimba itaibuka mshindi. Simba imeshatolewa,” anasema shabiki Imad Hassan wa Misri.

Shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Uche Nwokolo wa Lagos, anasema “Simba 0 Enyimba 3. Enyimba ndiyo timu ya sasa. Simba itafungwa kwenye uwanja wao. Nataka kuliambia benchi la ufundi lisichanganyikiwe. Hawana budi kwenda kule na kuishinda Simba. Hakuna kujihami ni mashambulizi tu.”

Shabiki mmoja, Segun wa Port Harcourt ndiye pekee anayeona kuwa mechi hiyo itaisha kwa sare ya bao 1-1 kwa kuwa anasema Enyimba imeshafanya kazi kubwa ya kushinda kwa mabao mengi nyumbani.

Hata hivyo, shabiki mmoja kutoka Tanzania, Msuya ametabiri kwenye tovuti hiyo kuwa Simba itashinda kwa mabao 7-0, akisema huu ni mwaka wa Simba.

Vigogo hao wa Nigeria wanatazamiwa kuwasili leo, ingawa taarifa za kuja kwao bado hazina uhakika.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments