Stars hoooi Kenya

Timu ya Taifa, Taifa Stars, jana Jumamosi ilianza vibaya michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani baada ya kufungwa na Kenya bao 1-0 katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, Kenya.

Stars waliokuwa wakicheza bila kuonana hasa katika nafasi ya ulinzi, walishambuliwa mara kadhaa na wapinzani wao ambao wengi wa wachezaji wao ni warefu.

Kwa mujibu wa matangazo ya moja kwa moja ya mchezo huo, bao la Kenya lilifungwa katika dakika ya 82 kwa kichwa na Antony Dafaa baada ya mlinda mlango Farouk Ramadhani kutoka kuuwahi mpira huo lakini akashindwa kuudaka.

Stars ilipoteza nafasi kadhaa za kufunga kupitia kwa Uhuru Seleman, Athuman Idd, Abdi Kassim na Fred Mbuna ambao mashuti yao yalikosa umakini.

Mrisho Ngassa aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Uhuru alibadilisha kwa kiasi kikubwa kasi ya mchezo wa Stars ambayo ilipooza mno kabla ya hapo.

Kocha Mkuu wa Stars, Marcio Maximo alisema wachezaji wake wa nafasi ya ulinzi hawakuwa na mawasiliano na Farouk hivyo kusababisha bao hilo, na pia alikiri katika kipindi cha kwanza wachezaji hawakuweza kumiliki mpira.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments