Kampuni ya Bia (TBL) kutumia mamilioni kufufua Taifa Cup Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) imewekeza mamilioni ya fedha kwenye Shirikisho la Soka (TFF), ikiwa ni katika mkakati wa kufufua msisimko wa michuano mikongwe ya Kombe la Taifa kwa kuiwezesha mikoa yote 23 ya soka kushiriki.

TFF na TBL, ambayo itatumia mashindano hayo kutangaza bia ya Safari Lager, juzi walisaini mkataba wa Shilingi bilioni 1.54 wa kudhamini mashindano kwa miaka mitatu.

Kati ya hizo, Shilingi milioni 580 zikitumika kila mwaka kuanzia mwaka huu ambao mashindano hayo yatakayofanyika Dar es salaam.

“Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya posho, malazi, usafiri wa kuja Dar es salaam na usafiri wa ndani wakati wa mashindano hayo,” alisema Meneja Masoko wa TBL, David Minja wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo kwenye hoteli ya Royal Palm Movernpick juzi usiku.

“Na ili kuongeza msisimko, bingwa atajinyakulia Sh milioni 30, wakati mshindi wa pili atapata Sh milioni 15 na mshindi wa tatu sh milioni 7.5.”

Zawadi nyingine zitakazotolewa ni kwa mwamuzi bora, ambaye atajinyakulia Sh milioni 2, mchezaji bora, mlinzi bora na mfungaji bora, ambao pia kila mmoja atajinyakulia Sh milioni 2.

“Lengo la Safari Lager ni kuhakikisha mashindano haya yanaleta msisimko Tanzania na kuinua vipaji vya soka,” alisema.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera aliipongeza TFF kwa kazi nzuri ya kuendeleza mchezo huo Tanzania na kusema kuwa lengo zaidi lielekezwe kwenye timu za vijana.

Bendera, pia alivitaka vyama vya mikoa kuchagua wachezaji wenye uwezo badala ya kuangalia sura, ukabila pamoja na kupeana safari na posho wakati mchezaji hana uwezo.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliipongeza TBL kwa hatua yakle ya kuendeleza mchezo huo kupitia udhamini wake kwani soka ya Tanzania na popote inaendelea kutokana na udhamini.

Tenga aliitaka mikoa kuunda timu imara kwa ajili ya kuibua vipaji pamoja na kuongeza ushindani kwenye mashindano hayo.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments