Kila la kheri Simba kesho dhidi ya Enyimba Nigeria

MABINGWA wa Soka Tanzania, Simba kesho watakuwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Aba, Nigeria kurusha kete nyingine dhidi ya mabingwa wa Nigeria, Enyimba katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba na Yanga ndizo zilizosalia kwa timu za Tanzania katika michuano hiyo ya klabu Afrika, baada ya Miembeni ya Zanzibar kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini wakati Chipukizi ilitupwa nje na Muffurila Wonderers ya Zambia katika Kombe la Shirikisho.

Yanga ilikuwa mjini Tripoli, Libya jana usiku ikicheza na Al Akhdar katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza wa Kombe la Shirikisho.

Simba inacheza na Enyimba ikiwa ni mechi yao ya tano kwa timu hizo kukutana, katika mchezo wa kwanza mwaka 2003, Simba ilichapwa mabao 3-0 na marudiano Simba ilishinda mabao 2-1, wakati mwaka 2005, Simba ilitolewa na timu hiyo baada ya kuchapwa mabao 4-0 mjini Aba kabla ya kutoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ushindi wa Simba katika mchezo wa kesho, utakuwa na faida kubwa mbili, kwanza kujenga heshima ya Simba na Tanzania kwa jumla na pia kuvunja mwiko wa timu hiyo kutofungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani. Enyimba iliwahi kufungwa mara moja tu mabao 2-1 na Al Ahly kwenye uwanja huo.

Ushindi wa Simba utaiweka klabu hiyo ya Tanzania kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele kwa mchezo wa marudiano ikitiliwa maanani kuwa bao la ugenini lina faida kubwa.

Vyombo mbalimbali vya habari Nigeria vimetangaza kuifanya mechi hiyo kuwa ya kitaifa na serikali ya Nigeria pia imetangaza kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali kuhakikisha inashinda mchezo wake huo na kuipaisha timu hiyo katika michuano hiyo Afrika.

Hakuna asiyejua ukubwa wa mkono wa serikali, siku zote mkono ni mrefu na unakuwa na mafanikio makubwa. Wengi tumeishuhudia Taifa Strars ikishinda mechi zake kutokana na kuwepo kwa mkono wa serikali pamoja na wadhamini wa haja.

Lakini pamoja na hayo, dua pekee ndiyo inayoweza kuyashinda hayo na ushindi kupatikana, kwa kuwa Mungu ndiye anayeweza kusikiliza yule anayemuomba la mafanikio.

Dua za Watanzania ndizo silaha zitakazozima nguvu ya mashabiki wa Nigeria na hata kuupinda mkono wa serikali hatimaye Simba kushinda mchezo huo.

Itakuwa unyonge usiyo mfano kwa Simba kupoteza mchezo huo kwa mara ya tatu kwenye uwanja huo tena kwa idadi kubwa ya mabao.

Kama alivyosema Katibu Mkuu wa timu hiyo, Mwina Kaduguda wakati akitoa mawaidha ya kuwaaga wachezaji hao juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jitihada za wachezaji wenyewe ndizo zitakazoleta ushindi.

Pia wanatakiwa kucheza kwa nidhamu na kufahamu kuwa mchezo wanaocheza ni tofauti na Ligi Kuu ya vodacom ambayo wakati mwingine huishia kwa waamuzi kufungiwa.

Umakini wa wachezaji, nidhamu ya hali ya juu, kucheza kwa malengo ya ushindi pamoja na dua zetu tuliobakia nyumbani ni ngao ya ushindi kwa Simba. Enyimba inafungika na Simba inaweza kushinda mchezo huo. Mungu ibariki Simba, Mungu ibariki Tanzania.

Imenakiliwa toka Gazeti la Mwananchi.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments