Hatma ya Stars kwa JK

Hatma ya maamuzi ya kutumia Uwanja Mpya wa Taifa kwa ajili ya mechi ya kwanza ya timu ya soka ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Mauritius, ambayo imepangwa kufanyika Mei 31 hapa nchini sasa iko mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Stars, ambayo, mwaka jana iliweza kufanya vizuri kwenye mechi za kuwania nafasi ya kushiriki fainali za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika na kutolewa katika hatua za mwisho kwa mara ya kwanza imepangwa kuanza katika makundi mwezi Mei kwenye mechi za kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 zitakazofanyika nchini Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana hapa jijini zinasema suala hilo sasa limefikishwa kwa Rais Kikwete kutokana na kuaminika kuwa na mamlaka ya kuweza kusaidia kumaliza tatizo hilo la kupata ruhusa ya kuutumia uwanja huo, ambao ndio umekaguliwa na wakaguzi wa Shirikisho la soka la dunia (FIFA).

Hatua ya suala hilo kupelekwa Ikulu limetokana na viongozi wa Wizara kushikwa na `kigugumizi` kuhusiana na Stars kutumia uwanja huo.

Chanzo hicho kimeendelea kusema kuwa licha ya wizara kusema kuwa hautaweza kutoa ruhusa ya kuutumia uwanja huo mpaka pale ujenzi wake utakapokamilika na kukabidhiwa na wakandarasi ambao ni kampuni ya Beijing Construction lakini bado kunaonekana kuwepo uwezekano kwa uwanja huo kukamilika mapema.

“Kumekuwa na kauli zinazopingana juu ya uwanja huo mpya, majibu rasmi hayajatolewa huku muda wa siku 90, ambao umepangwa na FIFA ili kuthibitisha jina la uwanja kwa sasa umeshapita, sijui itakuwaje,“ kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza kuwa licha ya mkataba wa ujenzi huo kuonyesha kuwa muda wa makabidhiano ni mwezi Juni lakini kuna uwezekano wa kuweza kumaliza zoezi la ujenzi katika sehemu iliyobakia kabla ya muda huo na kuweza kutumika katika mechi hizo za kimataifa.

Mwishoni mwa mwaka jana ujenzi wa uwanja huo ulisimama kutokana na madai kuwa awamu ya pili ya fedha za uwanja huo kuchelewa kutolewa na pia kuvunjwa kwa sehemu ya kukimbilia wanariadha ambayo ilikuwa imejengwa bila kufikia viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la riadha la kimataifa (IAAF).

benchi-la-taifa-stars.jpg

Stars pia kwenye michuano hiyo itakuwa inawania tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Angola, ambapo imepangwa kundi moja na nchi za Cameroon na Cape Verde.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments