Twiga Stars huu si mwisho wenu-mhariri wa mwananchi!

TIMU ya soka ya wanawake, Twiga Stars leo inashuka uwanjani mjini Yaounde Cameroon kucheza mchezo ambao unaweza kuwa wa kukamilisha ratiba kutokana na ukweli kwamba ilifungwa mabao 3-0 katika mchezo wa awali jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Inawezekana kuwa licha ya kuondoka juzi ikiwa na matumaini kuwa inaweza kushinda na kulipiza kisasi dhidi ya dada zao wa Cameroon, lakini matumaini yao ni madogo mno.

Kwa upande wetu, tunapenda kuiombea dua timu yetu ambayo ni wawakilishi wa Tanzania katika medani ya soka la wanawake kimataifa.

Tunapenda kuwatia moyo akina dada hao kwamba kufungwa kwao mabao 3-0 katika mchezo wa awali si mwisho wa wao kuweza kufanya vizuri katika mchezo wa soka.

Tunaamini kuwa Twiga Stars inapaswa kusaidiwa na kila mpenda michezo, hasa soka ili iwe timu ya kudumu na kutambua kwamba Tanzania inalo jukumu la kushiriki michezo mbalimbali ya kimataifa kwa wanawake katika siku za usoni.

Hilo, ndilo jukumu ambalo litakiwa kufuata baada ya mechi hiyo dhidi ya Cameroon na kwa uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lianze kubadilika na kuwa na mtazamo chanya kuhusiana na maendeleo ya mchezo wa soka kwa wanawake.

Pia, tunaamini kuwa soka ambalo limeonyeshwa na akina dada hao limeweza kuwa la kuridhisha, hivyo halitakuwa jambo la maana kwa TFF kuitupa na kuiacha kabisa timu hiyo ambayo imeanza kuionyesha dunia kwamba soka pia linaweza kuchezwa na wanawake wa Kitanzania.

Tunataka baada ya kurejea, TFF ikae chini na kufanya tathmini ushiriki wa Twiga Stars, iangalie akaunti ya timu hiyo, madeni ambayo shirikisho hilo limeingia kwa kuigharimia timu hiyo.

Kama ambavyo tuliambiwa wakati wa kuondoka kwa timu hiyo kwenda Cameroon kwamba tiketi zilikopwa kutoka kwa wakala wa shughuli za usafiri wa masuala ya ndege, lakini TFF haikusema wazi ni kiasi wafadhili waliichangia timu hiyo hadi inakwenda huko.

Tunasema kuwa itakuwa bahati mbaya kuiacha mitaani Twiga Stars na hasa wachezaji wake, badala yake, TFF iangalie suala la kuwa na ligi ya soka ya wanawake ambako vipaji vipya vitaweza kugundulika.

Tunashauri kwamba TFF inaweza kushirikiana pia na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kupitia michezo kama ile ya shule za sekondari (Umisseta) ambayo inatarajiwa kuanza upya, ili soka la wanawake nalo lipewe nafasi katika mchakato huo wa kimaendeleo.

Pia, taasisi binafsi kama ile ya Powell iliyoko Bagamoyo, Mkoa wa Pwani inayoendeshwa na mwanamichezo maaarufu nchini, Kanali Idd Kipingu inatumika kikamilifu kulea na kukuza vipaji vya wachezaji wakiwamo wasichana ambao hatimaye wanachukuliwa ili waichezee Twiga Stars.

Kwa wachezaji nao wakirejea, inafaa wasikate tamaa, watambue kuwa huo si mwanzo wao kuingia mitaani na kumalizika kimchezo, bali wale wanaotoka katika taasisi kama za kijeshi, waendelee kujinoa na kuendelea na mazoezi wakisubiri michezo ijayo kitaifa na kimataifa.

Kamwe wasikate tamaa kwani ni kosa kwa vijana kukata tamaa, hasa kwa mambo ambayo yanatokea katika sekta ya michezo kote ulimwenguni.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments