Simba `yaisafishia njia` Yanga


By Jimmy Charles

Simba jana imeifagilia njia Yanga ya kunyakuwa ubingwa baada ya kuichapa Prisons ya Mbeya 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania uliochezwa kwenye Uwanja wa taifa, jijini, Dar es Salaam.

Mchezo huo, hata hivyo, ulilazimika kuchezwa saa saba mchana ili kutoa nafasi kwa Televisheni ya kulipia ya GTV kurusha matangazo ya mchezo huo.

sports2.jpg

Mchezo huo ambao umelalamikiwa na wachezaji wa pande zote mbili kwa kuchezwa katika muda na kuwasababishia baadhi ya wachezaji maumivu ya miguu kutokana na nyasi bandia kuwa na joto kali.

Simba ikiwa imepoteza matumaini ya ubingwa, ilianza mchezo huo kwa kasi, ambapo wachezaji George Owino, Moses Odhiambo, Ulimboka Mwakingwe na Emmanuel Gabriel walionyesha uelewano wa hali ya juu kwa kulishambulia lango la Prisons mara kwa mara.

Iliichukua Simba, dakika 24 kupata bao la kwanza lililopachikwa wavuni na Gabriel baada ya kupokea pasi safi ya Ramadhani Wasso na kupiga shuti kali lililomshinda Kipa wa Prisons, Exavery Mapunda.

Wachezaji wa Prisons wakiwa katika mshtuko wa kufungwa, Gabriel alizamisha bao la pili dakika tano baadae kwa kuunganisha kwa kichwa krosi safi ya Odhiambo.

Katika kipindi cha pili, Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Mohamed Banka na nafasi yake kuchukuliwa na Nico Nyagawa katika dakika ya 56, ambapo mabadiliko hayo yaliisaidia Simba kwa kupata bao katika dakika ya 61 baada ya Nyagawa kupiga mpira mrefu uliomkuta Odhiambo, ambaye naye alipiga pasi safi iliyomkuta Gabriel na kupachika bao la tatu.

Baada ya kupachikwa bao hilo, Kocha wa Prisons Juma Mwambusi alifanya mabadiliko, ambapo alimtoa Oswald Moris na kumuingiza Henry Mwalugalu katika dakika ya 67, ambaye aliweza kuisadia timu yake kupata bao la kufutia machozi baada ya kupiga pasi nzuri iliyomkuta Mtupa, ambaye aliangushwa kwenye eneo la hatari na Said Nasoro na mwamuzi Pascal Chiganga wa Mara alitoa penati iliyojazwa wavuni na Yona Ndabila.

Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic alisema kuwa timu yake ilicheza vizuri wakati Kocha wa Prisons, Juma Mwambuzi alilalamikia joto kali lililosababisha wachezaji wake kuchoka.

Matokeo hayo yameifanya Simba kuruka hadi nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 27 huku ikitoa nafasi kwa Yanga kuendelea kukaa kileleni kwa kuizidi Prisons pointi moja.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments