Mkuchika Waziri mpya wa Michezo

Tanzaniasports::Where Sports People Meet


By Jimmy Charles

Rais Jakaya Kikwete amemteua Mbunge wa Newala George Mkuchika kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika baraza jipya la Mawaziri alilolitangaza jana katika Ikulu ndogo ya Chamwino mjini Dodoma.

Awali, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Mohamed Seif Khatib, ambaye sasa amekuwa waziri anayeshughulikia masuala ya Muungano.

Mabadiliko hayo ya wizara pia yamemkumba aliyekuwa naibu waziri wa wizara hiyo aliyekuwa akishughulikia masuala ya Habari na Utamaduni Daniel Nsanzugwako ambaye hajapewa wizara yeyote.

Aidha, Kikwete amemrudisha kwenye wizara hiyo Joel Bendera ambaye alikuwa chini ya Khatib, ambapo alikuwa akishughulikia masuala ya michezo.

“Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo ni George Mkuchika wakati Naibu wake ni Joel Bendera,“alitangaza Kikwete katika taarifa hiyo iliyorushwa moja kwa moja na televisheni ya ITV.

Aidha, Kikwete amepunguza idadi ya manaibu waziri wa wizara hiyo kutoka wawili kama ilivyokuwa awali na kubakiwa na naibu mmoja ambaye atashughulikia masuala yote kama ilivyo kwenye wizara nyingine.

Khatib, aliiongoza wizara hiyo kwa kipindi cha miaka miwili, ambapo katika uongozi wake alisaidia kurudisha mahusiano kati ya vyama vya michezo na serikali.

Mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri yamekuja kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa baada ya kutolewa kwa taarifa ya Richmond iliyomgusa yeye moja kwa moja.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments