Nidhamu Mbovu Yawaangusha Wanamichezo Wa Kitanzania

Kutokuwa na malengo na nidhamu mbovu ni sababu mbili kuu zinazosababisha wachezaji wa Kitanzania kushindwa kwenye majaribio ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo, BMT, na mmiliki wa shule ya sekondari ya Lord Baden Powell Memorial iliyopo Bagamoyo, ambayo kituo cha michezo cha soka kitakuwa ndani yake, Idd Kipingu alisema jijini katikati ya wiki kuwa wachezaji wengi wamekuwa hawana nidhamu na malengo, jambo ambalo linasabisha wanaowajaribu kushindwa kuwachukua kwenye timu zao.

Kipingu alisema wachezaji wengi ambao anawajua lakini alikataa kuwataja, wameshindwa majaribio kutokana na sababu hizo mbili kubwa.

Kule majaribio yapo ya aina nyingi. Mchezaji anaweza kuambiwa akimbie mita fulani na anapewa muda, au aruke koni au kucheza na mpira jinsi atakavyoelekezwa, alisema Kipingu.

Lakini akienda kinyume na hapo wenzetu wanachukulia nidhamu zao ni mbovu. Na pia hawana malengo kwani wangekuwa na malengo wangejitahidi kuonyesha uwezo wao wote.

Wachezaji wengi, hasa wanaocheza kwenye klabu za Simba na Yanga wamekuwa wakienda kufanya majaribio nje ya nchi lakini wakashindwa na kurejea. Baadhi wamepata mikataba ya kucheza kwa miezi michache kwenye nchi za Uarabuni.

Hatahivyo, Kipingu alisema kwa sasa tatizo hilo litamalizika baada ya kuanzishwa kwa kituo hicho ndani ya shule hiyo, inayochukua wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao wataanza kufundishwa sasa na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miaka minne.

Alisema wachezaji hao ambao watapata elimu ya sekondari katika shule hiyo, watafanya soka kama moja ya somo ambalo litawasaidia kujua mambo mengi.

Aidha wachezaji hao watakuwa wakifanya ziara za kila mwaka kwenye nchi za Ulaya ili kuwasaidia kufanya vizuri na watakaowavutia mawakala watauzwa huko.

Kigezo kikubwa cha kujiunga na shule hii ni lazima mtoto awe na kipaji cha kucheza soka na makubaliano yatafanyika kwa maandishi na wazazi, alisema Kipingu na kueleza zaidi na endapo itatokea klabu itakayomrubuni mtoto kuvunja mkataba, basi itashitakiwa kisheria.

Shule hiyo itakuwa na wachezaji 30, ambao walitarajiwa kupatikana juzi Ijumaa baada ya mchujo wa siku mbili uliofanywa na makocha kutoka kwenye timu ya Bolton Wanderers ya Uingereza uliohusisha wachezaji 100.

Kati ya wachezaji hao, 44 ni kutoka kwenye mashindano ya kwanza ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Copa Coca cola, na waliobaki walitoka wawili-wawili kila mkoa.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments