Yanga kurudia zoezi la utoaji fomu

Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imepanga kutoa fomu nyingine 30,000 za uanachama baada ya idadi kama hiyo za awali kuisha katika mikoa 10 tu.

Yanga ilisambaza fomu 30,000 za maombi ya uanachama lakini idadi hiyo imeishia katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Morogoro, Zanzibar na Dar es Salaam.

Yanga ilitoa fomu za maombi mapya ya uanachama mwezi uliopita kwa lengo la kuongeza wanachama wake kutoka chini ya 2000 waliopo sasa.

Mwenyekiti wa Yanga Iman Madega alisema jijini fomu zitakazoongezwa zitasambazwa kwa awamu katika mikoa ya Pwani, Tanga, Kagera, Mara, Kigoma, Tabora, Ruvuma, Rukwa, Singida, Lindi na Mtwara.

“Tumeona hili tatizo kwamba fomu tulizotoa awali zimekuwa chache,“ alisema Madega na kueleza, “baada ya mchakato wa hizi za kwanza, tutatoa nyingine kipaumbele kikiwa mikoa ambayo haikupata awali.“

Ili kupata uanachama wa klabu hiyo, mwombaji anatakiwa kununua fomu hizo kwa sh. 1,000 kwenye matawi ya Yanga na baada ya kukubaliwa na kamati inayoshughulikia zoezi hilo, muombaji atatakiwa kulipia sh. 14,000 zikiwa ni ada ya mwaka mmoja na kadi.

Kutokana na uuzaji wa fomu 30,000 za awali, klabu hiyo itaingiza sh. milioni 450.

Madega alisema awamu ya pili ya usambazaji wa fomu itafuata baada ya kumalizika kupitiwa kwa fomu za awamu ya kwanza kutokana na gharama kubwa iliyopo katika kazi hiyo.

“Ni gharama sana kusambaza hizi fomu maana wenye kufanya shughuli hii lazima walipwe posho kwasababu wanakopeleka sio mikoa yao.

Wanahitaji malazi, chakula na usafiri kwa siku zote watakazokaa huko,“ alisema Madega.

Wasambazaji wa fomu hizo katika awamu ya kwanza wamelipwa posho ya sh. 45,000 kwa siku wanazokuwa safarini.

  • SOURCE: Lete Raha

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments