Je Tunahitaji Viongozi wa Aina gani Katika Michezo

Hivi karibuni tumeshuudia kauli nyingi za wapenzi na wadau wa michezo wakitaka mabadiliko katika uongozi wa vyama vyetu vya michezo.

Ni kweli na nakubaliana nao kuwa uongozi wa vyama vyetu vya michezo vinahitaji mabadiliko makubwa ili kuwepo na msukumo wa kweli wa michezo hapa nchini.

Kuteuliwa kwa Mheshimiwa Joel Bendera ( MB )takribani miezi kumi sasa kulileta faraja kubwa kwa wapenzi na wadau wa michezo nchini.Kwa ufupi matarajio mengi mazuri yanategemewa kutokana na uteuzi huokatika sekta hiyo ya michezo.

Licha ya kuwa mwanamichezo wa muda mrefu Ndugu Bendera pia ni mtaalamu aliyebobea katika sayansi ya michezo kutoka Chuo Kikuu cha Leipzig Ujerumani. Binafsi nakifahamu chuo kutokana na umaarufu wake na pia kuwepo hapo kwa takribani mwaka mmoja. Leipzig University kimetoa wataalam wengi kwa nchi kama Mozambique Angola,Ethiopia, Eritria, Guinea, Cape Verde na nchi nyingi za America ya Kusini.Sishangai hata kidogo kuziona nchi kama Angola Ethiopia na Mozambique zikitunyanyasa kimichezo.

“Vision” ya nchi hizo katika nyanja za michezo kwa ujumla ni tofauti kabisa na sisi tuendako. Viongozi wetu wengi ni wababaishaji. Haikunistua kuona hivi karibuni mmoja ya viongozi wa nafasi ya juu kusimamishwa kwa kudanganya matumizi ya chama chao.

Binafsi nakumbuka kukipatia chama fulani Tshs 15 million kwa niaba ya kampuni niliokuwa nikitumikia kwa masharti ya kupatiwa mahesabu mara tu wamalizapo mashindano. Kilichotokea ni aibu kwani zaidi ya asilimia hamsini ya pesa hizo zilitumika bila ya maelezo ya kuridhisha.

Hao ndio aina ya viongozi tulionao hivi sasa.Bahati nzuri mlezi wa chama hicho alikemea sana suala hilo siku aliyokuwa akiacha ulezi wa chama hicho.Mlezi huyo aliwaasa viongozi wa mchezo huo kuwa waadilifu na wabunifu kama kweli wanataka kuongoza mchezo huo.

Kwa maoni yangu viongozi tunaowahitaji wawe kama ifuatavyo;
(1) Tunahitaji viongozi wenye mipango mizuri ya maendeleo
(2) Tunahitaji viongozi wenye uwezo wa kutafsiri mipango hiyo kwa ufasaha na kutenda.
(3) Tunahitaji viongozi wenye mwelekeo wa maendeleo
(4) Tunahitaji viongozi wanaoweza kupata heshima ya wale wanaowaongoza
(5) Tunahitaji viongozi wenye kufuata maadili mema ya uongozi
(6) Tunahitaji viongozi wakweli na waaminifu

Labda sio rahisi kupata viongozi kama malaika lakini nina imani Tanzania inao viongozi walio wakweli au wawazi katika uendeshaji wa shughuli wa vyama vyao.Kamwe viongozi wababaishaji wasipewe nafasi katika chaguzi za vyama vyetu.
Tunahitaji viongozi watakaojiuliza siku moja nini wamefanyia vyama vyao kwa niaba ya nchi na sio wale ambao wanasubiri kuona wameneemeka vipi na uongozi wa michezo.

Kwa mantiki hii nawakumbuka sana akina Wilbard Kente waliowahi kutuletea mashindano makubwa ya mpira wa vinyoa -Badminton barani Afrika chini ya jina la Mwalimu Nyerere.

Pia nawakumbuka watu kama Twaha Khalfan aliyewahi kuwa naibu mkurugenzi michezo aliyeamua kuongozana na timu ya mpira wa wavu hadi Lusaka Zambia kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki naKati . Mshangao wangu kwake ni kutokana na kukataa tiketi ya ndege na kuamua kusafiri nasi kwa treni ili ajue adha tutakayopata njiani hadi Lusaka

Mwisho ni mategemeo yangu Baraza la michezo la Taifa chini ya uongozi wa Ndugu Kipingu litaona umuhimu wa kusimamia kikamilifu maendleo ya michezo nchini na kuhakikisha lengo la serikali yetu linafikiwa katika fani ya michezo.

Ndugu Muharram Mchume ni Katibu mkuu wa kwanza wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania Tava na pia ni mkurugenzi wa mafunzo ya utawala kamati ya olimpiki Tanzania

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments