Jee michezo ni soka pekee?

Maneno mengi yamekuwa yakisemwa kuhusu Awamu ya Nne na Rais Jakaya Kikwete juu ya michezo na wengi wakiisifu Serikali hiyo na Rais kuwa imepania kufufua, kuinua na kujenga michezo ndani ya nchi.

Sifa hizo zimeenea, au tuseme zimeenezwa lakini tupo wengine hatuamini kuwa kuna nia ya Serikali na Rais Kikwete kukuza michezo, isipokuwa tumekuwa tukiona na tumethibitisha kuwepo kwa kila dalili kuwa kinachopiganiwa na kupewa umbile ni mchezo mmoja tu, nao ni mpira wa miguu.

Jambo hilo halitaki tochi chembilecho vijana maana kila linalofanywa au lilofanywa na Serikali ya Kikwete tokea kuingia madarakani basi ni kuhimiza mchezo huu kama kwamba kweli utaweza kunawa uso wa nchi hii, ilhali tukijua hilo ni gumu kutokea.

Ni gumu kama tuivyoona hivi juzi pale timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars ilipopigwa kumbo na Msumbji kwa kufungwa bao 1-0 na kumaliza tama ya nchi hii kucheza katika fainali za soka za barani Afrika kwa mara ya pili katika historia ya taifa hili.

Ilikuwa wazi kwamba Tanzania haikuwa na nafasi ya kwenda Ghana mara baada ya kutoka sare 1-1 na timu ya Senegal katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Kirumba, Mwanza na kuwa Watanzania walikuwa wanajidanganya kuwa ushindi dhidi ya Msumbiji itakuwa ni kufunguka mlango wa kwenda Ghana ilhali wakijua kuwa Senegal wanacheza nyumbani kwao, tena na timu ambayo haina tama tena.

Matokeo ya mechi hiyo ni zaidi ya bilioni 5 zilotumika kuitayarisha, kuisafirisha, kuiletea mechi za kujipima, maposho ya wachezaji, bakhshishi za Wabunge na kadhalika, zote hizo zimeingia chooni.

Tupo sisi tuliopinga timu ya taifa Taifa Stars kupelekwa Bungeni baada ya kuifunga Burkinafaso tukisema kuwa kitendo hicho hakina maana kwa sababu hicho kinachofurahiwa kitakuwa si chochote iwapo timu haitafuzu kwenda kucheza Ghana.

Na hapa ndipo penye moja ya hoja yangu kuu kuwa Serikali ya Rais Kikwete inaupa mpira wa miguu umuhimu mkubwa kupita kiasi kwa hasara ya michezo mengine mingi ambayo ina fursa zaidi kuliko soka kuliletea furaha taifa hili.

Kwa fikra zangu, kitendo cha kuipeleka timu Bungeni kilikuwa ni cha kisiasa na kwa kweli wanasiasa walikitumia vizuri sana, lakini hakuna la maana lilofanywa katika kuikuza hata hiyo soka, inayopewa umuhimu wa juu na Serikali na Rais Kikwete.

Tizama ziara zote za Kikwete ambapo alipata nafasi ya kwenda kwenye taasisi za michezo. Ni uwanja wa Real Madrid na Newcastel United na ikaishia nchi hii nzima kutikisika kuwa timu ya Real Madrid itafanya ziara ya kimichezo ya Tanzania, na ndoto hiyo ikayayuka kama siagi iliopitishiwa kisu moto.

Tizama Rais anavyohudhuria michezo ya mpira wa miguu na hata kupata wasaa wa kuzungumza na wachezaji wa Taifa Stars na kuwaalika wale na yeye na jiulize amewahi kupata nafasi ya kuiaga timu ya taifa ya Tanzania iliyokwenda Algiers kwa ajili ya michezo ya Afrika?

Tunaamini kocha Marcio Maximo analipwa mshahara wa kiasi cha dola 35,000 kwa mwezi na wakati huo huo ameajiriwa kocha mwengine wa timu ya taifa ya vijana ambaye hatujui nae analipwa malukuki mangapi ya shillingi.

Ukitizama fursa ambazo amepewa Maximo za kumrahisishia kufanya kazi yake, hazijawahi kutolewa kwa mtu au timu yoyote nyengine, hata iwe inakwenda kwenye michuano ya Olimpiki.

Kama kuna kocha mwengine yoyote wa mchezo mwengine wowote ule basi halipwi na Serikali bali ni msaada kutoka nchi rafiki na hiyo ikimaanisha kuwa tumeletewa kocha wanaotaka wao na sio tunaemuhitaji kwa vigezo vyetu.

Katika hali kama hiyo michezo mengine inafanywa kuwa ni watoto wa kambo maana baba yao hana nafasi ya kuiona seuze kuijua kabisa na sisi tunaamini kuwa hilo si jema kujenga mapenzi na uwiano baina ya michezo mbali mbali ndani ya nchi.

Picha inayoonekana kwa Kikwete basi inatoa nuru yake katika muundo wa Wizara inayosimamia michezo ambayo hatusiti kusema kuwa nayo imelalia mchezo wa mpira wa miguu zaidi kuliko michezo mengine.

Kuna michezo mingi ambayo tumezoea kuiita midogo ambayo inaweza kuisogeza nchi ikafika pazuri katika ramani ya michezo duniani. Kinachogomba na mapenzi kupita kiasi ya mpira wa miguu na woga wetu wa kujaribu kitu kipya.

Tizama mchezo kama mpira wa wavu ambao hivi sasa umeifunulia Kenya pazia jengine la michezo. Timu ya Kenya imejipatia jina kubwa duniani na hata kama mara hii haitafikia fainali za dunia huko Osaka, lakini bado sasa nchi hiyo ni miongoni mwa miamba ya mpira wa wavu Barani Afrika na inajulikana duniani.

Mchezo kama mpira wa vinyoya zama zile za kuongozwa na Wilard Kente na wachezaji maarufu kama Nasra Juma, Muhamed Juma, Ali Abeid, Nasor Juma, Juma Reli na wengine na timu ya Tanzania ilipofikia katika kiwango cha mchezo huo Barani Afrika.

Tizama mchezo wa mpira wa meza zama zile za akina Abdulawakat Juma, Nariman Jidawi, Muhammed Salim Shaaban Muhammed, Issa Khatiba, Issa Mtawazo, Bimkubwa Suleiman nchi hii ilivyokuwa ikitamba kwa mchezo huo wa mpira wa meza.

Kwa kuwa na vikosi imara vya kijeshi, penye mipango mizuri nchi hii inaweza kuwa mbele kabisa katika mchezo wa kutunga shabaha ambao unashindaniwa katika Olimpiki na timu za Kizungu zinajipatia medali zao za ziada kwa michezo kama hiyo ya shabaha, ambapo sisi tumeshindwa kutumia fursa tulizonazo.

Mchezo kama sataranji au chess usiokuwa na gharama kubwa katika uwekezaji, ambapo una Olimipiki yake peke yake, una fursa kubwa ya kuiletea fursa nchi hii, lakini bidii yoyote haijafanywa na hata sijui kuwa kuna viongozi wengine katika Wizara ya Michezo wanajua kuwa kuna mchezo kama huu.

Yote ya kuipa kisogo michezo mengine inatokana na imani kuwa ukombozi wa michezo wa nchi hii utakuja kwa kupitia mpira wa miguu na si chengine chochote kile.

Ukweli mmoja hatuukatai nao ni kuwa mchezo wa mpira wa miguu una fursa kubwa duniani na aina ya marejesho ya kifedha ni makubwa kuliko kwa mchezo mwengine wowote iwapo mchezaji atafanikiwa kufikia kiwango cha juu kinachohitajika.

Lakini kufika huko ni mbali sana maana mchezo huo tukubali kuwa una ushindani mkubwa pia, na ushindani huo unazidishwa na mfumo wa mazoezi ambao wachezaji wetu watakuwa wanauota tu.

Kinyume chake, wachezaji wetu wa riadha wengi wamefanikiwa kufikia kiwango sawa na wachezaji wa Ulaya na majina kama ya Nyambui, Shahanga na mengine mengi sio tu yameleta sifa kwa Tanzania bali wachezaji hao wamefaidika kifedha na maslahi yao.

Tunachotaka kusema hapa ni kuwa kama kuiletea sifa nchi hii, basi ni riadha ndio imefanya hivyo, lakini bado hivi sasa haina kocha yoyote wa kigeni wa kulipwa hata dola 1,000 kwa mwezi seuze wa kulipwa dola 35,000 na pia kupewa mtaalamu wa viungo pia kama ilivyo kwa Taifa Stars.

Kushinda kwenda Ghana wengine tunaona ni zinduo. Zinduo la kukaa chini na kupanga upya vipa umbile katika michezo yetu, kupanga wapi pa kutia mkazo na wakati gani na pia kufikiria vipaji vyetu vinavyopotea kabla ya kukua na kujulikana.

Haiwezekani na haiingii akili hata kidogo kwa nchi yenye watu millioni 37 iwe tiro au isitajikane kabisa kwa michezo, Haiingia akilini hata kidogo kuwa nchi hii inadorora katika michezo na kuwa hakuna hata mchezo mmoja Tanzania inayotikisa.

Wakati umefika basi wa kuhakikisha kuwa tunatizama kwa makini na kutoa fursa zinazostahiki kwa michezo mengine ili nayo ithibitishe kuwa pawapo na nyenzo na fedha basi rasilmali watu yaani wana michezo wa hiyo michezo mengine watarudisha tija kwa taifa kuwekeza kwao.

Tujaribu basi tuone, kuliko kila siku kutia fedha kwa mchezo mmoja na ambao nao hauleti furaha kwa nchi hii.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments