Manchester City waiangamiza Newcastle

Manuel Pellegrini ameanza vyema ndoto yake Manchester City, baada ya kupata matokeo mazuri kuliko timu zote kwenye mechi ya kwanza.
Vijana wa City wamewakung’uta Newcastle United mabao 4-0 na kuanza kwa kushika usukani wa ligi, kwenye mechi iliyopigwa dimba la Etihad usiku wa Jumatatu.
Newcastle wanaofundishwa na Alan Pardew wanaweza kusema walicheza watu 10 baada ya Steven Taylor kutolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini walizidiwa kwa kila hali na Man City.
City walianza mchezo kwa kasi, ambapo Edin Dzeko alimpatia David Silva majalo safi ambayo hakukosea kuitia kimiani kufungua kitabu cha mabao dakika ya sita tu.
Mpachika mabao Sergio Aguero alidhihirisha umakini wake dakika ya 22 kwa kumtungua kipa Tim Krul kabla ya Taylor kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumkata kwanja Aguero.
Yaya Toure alifunga kwa mpira wa adhabu ndogo katika dakika ya 50 kabla ya Samir Nasri kukomelea jeneza la Newcastle kwa msumari wa mwisho katika dakika ya 75.
Wachezaji Fernandinho na Jesus Navas waliosajiliwa msimu huu walianza kipindi cha kwanza na walicheza vyema muda wote, wakati Alvaro Negredo aliingia kipindi cha pili, akatikisa nyavu lakini akaambiwa alikuwa amejenga kibanda hivyo likakataliwa.
Kipa wa Newcastle, Krul alionekana kuwa katika kiwango kizuri kimchezo, na ndicho kiliwazuia vijana wa mhandisi Pellegrini kupachika mabao zaidi. Historia inaonesha, hata hivyo, kwamba City wameshinda mechi zao zote nane zilizopita dhidi ya Newcastle, hivyo bado Pellegrini ana mitihani mingi anuai.

Enhanced by Zemanta

Comments