in , ,

Bado tuna ushamba kwenye soka!

Mchezaji wa timu ta Taifa kutoroka Nchini..

Wachezaji watovu kupunguziwa adhabu..

 

ENZI zile, nyumbani Tanzania lilikuwa si jambo la ajabu kwa wachezaji wa soka kutwangana masumbwi uwanjani,ugomvi ukaamuliwa na mechi kuendelea! Usingeshangaa enzi hizo,mwamuzi kupigwa na mchezaji au wachezaji. Hata kama kulikuwa na adhabu, lakini cha kushangaza ilikuwaje wachezaji waliamua tu kupigana au kupiga waamuzi?

Tukikumbusha matukio mabaya ya hivyo, mwezi Juni mwaka 1972, pambano la Yanga na Simba la fainali ya ubingwa wa Tanzania lilivunjika Yanga ikiongoza 1-0 kwa bao lililofungwa na winga hatari wa kulia Leonard Chitete (marehemu). Kisa cha kuvunjika kwa pambano hilo kilianza kwa mchezaji Emmanuel wa Simba kumpiga teke Gibson Sembuli (marehemu) wa Yanga na vurugu kubwa kutokea kwa wachezaji wa timu hizo kupigana. Katikati ya vurugu hizo, mabeki wawili wa kutumainiwa wa Simba Mohammed Kajole na Omar Choggo (wote marehemu) walijeruhiwa kwa virungu na askari wa mgambo. Walikimbizwa hospitali.

Angalia, licha ya tafrani kubwa yote hiyo, mwamuzi Manyoto Ndimbo aliziita timu zirudi uwanjani kumaliza mechi lakini Simba waligoma kutokana na pengo la Kajole na Choggo. Yanga wakatangazwa washindi na nahodha Abdulrahman Juma akakabidhiwa kombe na mgeni rasmi aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi aliyekuwa madarakani kwa takriban miezi miwili mpaka siku hiyo kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume kilichotokea Mwezi Aprili mwaka huo ambapo Jumbe alipewa nafasi yake.

Mwaka 1977, pambano “la kirafiki” la Pan African na Simba lilivunjika baada ya wachezaji wa pande mbili kupigana hovyo hovyo huku Abdallah Kibaden wa Simba ambaye ni kocha wa timu hiyo kwa sasa akichaniwa jezi raru raru! Takriban mwaka mmoja baadaye wachezaji watatu wa Simba ambao kwa sasa wote ni marehemu, Kajole, Adam Sabu na Jumanne Hassan Masmenti walimpiga mwamuzi wa mechi yao na Coastal Union ya mashindano ya kugombea kombe la sherehe za mwaka mmoja wa CCM kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma. Wachezaji hao walifungiwa mwaka mmoja na FAT ya Said Hamad El Maamry.

Waliokuwepo miaka ya 1970 mwishoni na 1980 mwanzoni watakumbuka jinsi kipa mahiri Juma Pondamali alivyokuwa akiwaumiza waamuzi kwa kipigo. Hayo ndiyo maisha yetu kwenye enzi ile ya ushamba katika soka. Leo hii kwenye dunia iliyostaarabiki haielezeki kwa wachezaji wa Yanga tarehe 10/3/2012 kumpiga mwamuzi wa pambano lao na Azam walilolala 3-1. Haielezeki zaidi kwa mchezaji Steven Mwasyika aliyempiga mwamuzi kupunguziwa adhabu mpaka kukosa mechi chache tu zilizobaki kabla ya msimu kumalizika tarehe 6/5/2012 siku 57 tu! Zaidi ya hayo, ilishangaza sana pale Yanga iliposimama kidete kumtetea mchezaji wa ajabu kama huyo! Hayo yalitendeka kwenye dunia hii? Tanzania iko wapi kwenye dunia ya sasa?

Tuhame hapo na kuanza tena nyuma kabisa. Enzi zile wachezaji walikuwa wanatoroka na kwenda Dubai (Jamhuri ya Falme za Kiarabu) kucheza soka ya kulipwa. Mara nyingi walikuwa hawaagi wala kuomba ruhusa, bali ghafla utasikia mchezaji katoroka ameenda Uarabuni. Wimbi la utoro huo lilishamiri sana kati ya mwaka 1976 mwishoni na mwaka 1986. Kipindi hicho mchezaji aliweza kutoroka na akacheza mpira Dubai! Hakukuwa na uhamisho wa kimataifa wala malipo yoyote kwa klabu. Lakini kwa mifumo yetu ya sasa hivi, jambo hilo ni ndoto kutekelezeka kwani lazima uhamisho wa kimataifa ufanyike kwa taratibu rasmi zilizowekwa.

Cha kushangaza sana, leo hii mchezaji wa soka wa Tanzania, Mwinyi Kazimoto, anatoroka kwenye kambi ya timu ya taifa na kwenda Qatar kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa! Hii imekaaje sijui, angefuzu majaribio huko angehamishwaje wakati hakuwa na baraka za klabu yake ya Simba? Na kwa kutoroka akiwa kambi ya timu ya taifa, chama cha soka cha nchi yake kingeshughulikiaje uhamisho huo? Huyu ameturudisha enzi ile wachezaji walipokuwa wanakimbilia Uarabuni watakavyo. Lakini kwa mazingira ya sasa, hilo halitekelezeki, bali utaenda popote kwa taratibu za uhamisho tu.

Tunamaliza kwa kutoa rai kwamba ushamba wetu kisoka ya sasa udhibitiwe ili twende vizuri kama dunia ya sasa inavyoenda. Hilo litawezekana kama viongozi wetu wa soka watalisimamia inavyopaswa. Baada ya mchezaji wa Yanga, Steven Mwasyika, kumpiga mwamuzi mwaka jana mwanzoni, angepata adhabu kubwa inayowiana na ubaya wa tendo hilo lisilo la kawaida kwa dunia ya sasa, wachezaji wengine wangeliogopa tendo hilo lakini kwa adhabu ndogo vile, sitashangaa tendo hilo la ajabu likijitokeza tena. Lawama hapa ni za viongozi waliomuadhibu kidogo Mwasyika kwa kosa kubwa.

Mchezaji Kelvin Yondani alitoroshwa usiku na kiongozi wa TFF toka kambi ya timu ya taifa kwenda kusaini mkataba na Yanga lakini hakuna hatua yoyote aliyochukuliwa kiongozi huyo, sasa mshangao unatoka wapi kwa Mwinyi Kazimoto kuipata pasi yake ya kusafiria akiwa kambi ya timu ya taifa wakati tunaambiwa wakiwa huko pasi hizo huwa hawanazo mikononi? Kiongozi aliyefanikisha utoro wa Kazimoto angeogopa nini wakati Yondani alipotoroshwa usiku toka kambi ya timu ya taifa hakuna hatua zilizochukuliwa kwa kiongozi aliyehusika?

Hebu jamani tuongeze umakini kwa mipango yetu ili tusiwe katika mambo mengi ya soka tukirudi kwenye miaka ya 1970 ,miaka takriban 40 nyuma, wakati dunia ikiwa kwenye miaka ya 2010 na ikisonga mbele. Watanzania tuache ushamba kwenye taratibu zetu za soka na utawala wetu wa mchezo huo.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Spurs kumpoteza Gareth Bale?

Manchester United: Kelele za nini?