Michezo yote 10 ya wiki ya nne ya EPL imeshachezwa. Kwenye makala hii mwandishi wetu amechagua kikosi cha wachezaji 11 waliofanya vizuri kwenye michezo ya EPL wiki hii.

Golikipa: TIM HOWARD (Everton)

Ni wazi kuwa alikuwa ni nyota wa mchezo dhidi ya Totteham hapo juzi. Alikuwa makini kiasi cha kutosha golini na akaokoa mashuti kadhaa ya washambuliaji wa Spurs likiwemo lile shuti zuri la Mason na kuufanya mchezo kubaki bila mabao.

Mlinzi wa Kulia: JOEL WARD (Crystal Palace)

Eden Hazard hakufurukuta kwenye mchezo wa hapo juzi dhidi ya Crystal Palace. Alikuwa ni Joel Ward aliyemzima nyota huyo wa Chelsea dakika zote za mchezo. Zaidi ya hapo akaifungia timu yake bao la ushindi kwa kichwa safi mwishoni.

Mlinzi wa Kati: WINSTON REID (West Ham)

Aliiongoza vyema safu ya ulinzi ya West Ham dhidi ya Liverpool hapo juzi. Aliyazima mashambulizi ya Liverpool kila walipokaribia langoni na akamfanya golikipa asiwe na kazi ya kufanya . Aliwazuia Benteke na Coutinho na hawakuleta madhara.

Mlinzi wa Kati: DAMIEN DELANEY (Crystal Palace)

http:/https://www.youtube.com/watch?v=ybijnu8-3UM

Alikuwa mwepesi mno kufanya kazi yake kila alipohitajika kwenye mchezo dhidi ya Chelsea hapo juzi. Aliwazuia vyema washambuliaji wa Chelsea hasa Diego Costa kila alipojaribu kushindana naye kwenye mipira ya hewani.

Mlinzi wa Kushoto: CHARLIE DANIELS (Bournemouth)

Ingawa mlinzi huyu ilibidi atolewe mapema kwenye kipindi cha pili cha mchezo lakini kiwango alichoonyesha kwenye kipindi cha kwanza kilitosha kabisa kumuingiza kwenye timu hii ya wiki. Krosi yake ndiyo iliyozaa bao la Bournemouth.

Kiungo wa Kati: FERNANDINHO (Manchester City)

Si rahisi kumuacha mchezaji huyu kwenye kikosi cha wachezaji 11 waliofanya vizuri kwenye michezo ya wiki hii. Hata asingefunga bao bado namna alivyotawala eneo la kiungo dhidi yaWatford kungetosha kumuweka kwenye kikosi hiki.

Kiungo wa Kati: MANUEL LANZINI (West Ham)

Kiungo huyu Muargentina alikuwa tatizo kubwa dhidi ya walinzi wa Liverpool kwenye kipindi chote cha mchezo. Alionyesha ubora wa hali ya juu kutokana na morali aliyokuwa nayo na hatimaye akachangia ushindi mnono wa West Ham.

Kungo wa Kulia: ANDRE AYEW (Swansea City)

Hakuna ubishi kuwa alikuwa nyota wa mchezo dhidi ya Manchester United hapo jana. Alifunga bao lake la tatu katika mchezo wa nne na pia akatengeneza lingine la ushindi kupitia pasi nzuri aliyopenyeza kwa Bafetimbi Gomis.

Kiungo wa Kushoto: RAHEEM STERLING (Manchester City)

Kwa mara nyingine winga huyu kijana ameendelea kuonyesha ni kwanini alisajiliwa na Manchester City kwa dau kubwa kiasi kile. Aliwapa tabu mno walinzi wa Watford kutokea upande wa kushoto. Alistahili kupata bao lake la kwanza hapo juzi.

Mshambuliaji wa Kulia: BAKARY SAKO (Crystal Palace)

Alichokifanya juzi dhidi ya Chelsea kitamshinikiza Jose Mourinho kuendelea kutafuta mlinzi kwa gharama yoyote sokoni haraka iwezekanavyo. Alifunga bao safi na akatengeneza lingine lililofungwa na Joel Ward.

Mshambuliaji wa Kushoto: DUSAN TADIC (Southampton)

Kiuhalisia Tadic ni Kiungo Mshambuliaji. Hata hivyo kwa namna ya uchezaji wake hapana shaka ana uwezo wa kusimama mbele zaidi na akafanya vizuri. Hapo jana aliwaangamiza Norwich kwa mabao yake mawili ya haraka katika kipindi cha pili.

 

 

 

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

TUNAHITAJI TFF YA NAMNA HII

Tanzania Sports

Ni lawama tu