in , ,

FIFA SASA YAPEWA URAIS WA TANZANIA!

UKIINGILIA masuala ya soka per se, unatafuta vita na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) hata kama wewe ni nani katika nchi yako uliye nje ya uongozi wa soka wa nchi.

 

Zaidi, wewe ukiwa serikali ndiyo kabisa hutakiwi kuingilia soka ya nchi yako, lakini unaweza kumlipa kocha wa taifa, kulipia kambi ya timu ya taifa, kusafirisha timu ya taifa kwenda nje ya nchi kushiriki mashindano na kadhalika.

 

Maamuzi ya watu wa soka kwa soka yao usiyaguse hata wakifanya maamuzi ya ajabu na ya ujinga uliopitiliza! Hivi ndivyo unavyoweza kuyaeleza kwa ufupi “maagizo” makali ya FIFA kulinda soka yao duniani dhidi ya dola za nchi.

Logo
Logo (Photo credit: Wikipedia)

 

Kimsingi, soka sasa inaonekana kuwa ni mhimili unaojitegemea wa nchi, kwani hata ikijadiliwa bungeni maazimio ya Bunge ili yatekelezwe, lazima utekelezaji huo ufanywe na Serikali au Mahakama wakati Serikali haitakiwi kuingilia masuala ya soka, huku masuala hayo yakiwa hayapaswi kufikishwa wala kuamuliwa mahakamani.

 

Kwa msingi huo, mihimili yote ya dola imefungwa mikono kuweka sawa masuala ya soka yanapovurundwa na kufumbiwa macho na watu wa soka wenyewe au uvurundaji huo unapofanywa kwa maslahi ya wenye sauti miongoni mwa watu wa soka.

 

Katika utaratibu wa mgawanyo wa mamlaka (separation of power) miongoni mwa Serikali (executive), Bunge (legislature) na Mahakama (judiciary), kuna utaratibu wa kudhibitiana (check and balance) ili mhimili mmoja usitumie mamlaka yake ovyo ovyo kwa kujiona hauna wa kuhoji utendaji wake. Bunge linajadili na kutoa maazimio dhidi ya serikali na mahakama zinapotenda kinyume, ambapo kwa mahakama si kwa jinsi zilivyoamua kesi.

 

Mahakama zinatafsiri sheria za Bunge na kutengeneza misingi mipya ya kisheria katika kutafsiri huko na zinaamua kesi za utawala dhidi ya serikali kwa kuweka misingi mizuri ya kisheria ya utawala bora. Serikali nayo ina mchango katika uongozi wa Bunge kwa kupitia kwa kiongozi wake bungeni ambaye ni waziri mkuu.

 

Aidha, Serikali yenyewe ndiyo hupeleka miswada bungeni ya kupitishwa kuwa sheria. Kwa upande mwingine, Serikali ni mteuzi wa majaji ili kuhakikisha mhimili wa Mahakama unakuwa na watenda haki walio bora. Kwa bahati mbaya kwa soka, hakuna udhibiti huo toka mhimili wowote wa dola baada ya zuio la FIFA kwamba soka  isiingiliwe.

Kimsingi, ni sahihi sana kuzuia soka isiingiliwe kwani hali hiyo ingeruhusiwa, mambo mengi ya soka yangechelewa kwani kila mara, kila chombo kingekuwa kinakuja na maelekezo yake ya nini kifanyike lini na hata mahakama zingetumika kusimamisha mashindano kwa amri ya muda (injunction) mpaka uamuzi fulani utolewe. Hapo hata kalenda za soka zingekuwa matatizoni.

Lakini sasa kinachokera ni kwa maelekezo hayo ya FIFA kutumika Tanzania kana kwamba FIFA hiyo sasa ni rais wetu namba moja anayesaidiwa na namba mbili wake, Jakaya Mrisho Kikwete katika masuala yoyote yanayogusa utawala wa soka hata kama si ya soka per se! Mfano wa hivi karibuni ni wa suala la serikali kupinga utaratibu wa uandikwaji wa katiba mpya ya TFF.

Hili ni suala la kukumbushana kufuata sheria za nchi na si suala la soka. Kama katiba iliyopo inatengeneza hali ya ulazima (mandatory) wa katiba mpya kutengenezwa na mkutano mkuu, ikitengenezwa kwa kuipitisha kwa wajumbe wa mkutano mkuu kuisoma na kuamua (secular resolution) inakuwa imetengenezwa kinyume cha katiba isipokuwa tu katiba hiyo ikiwa kimya kwa hilo.

Hata kwa tafsiri ya maneno kwenye katiba, ‘mkutano mkuu’ kwa tafsiri ya kisheria ni tofauti na ‘wajumbe wa mkutano mkuu’. Mkutano Mkuu ni mkusanyiko wa mahali fulani na wajumbe wa mkutano mkuu ni watu wanaoweza kuwa pamoja au walio sehemu mbalimbali.

 

Katiba ikisema katiba itapitishwa na mkutano mkuu, lazima ipitishwe na mkusanyiko mmoja wa wajumbe, lakini ikisema itapitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu inaweza kuwa kwa mkusanyiko au kwa kuipitisha kwao waitolee maoni kwa kuwaendea kokote waliko bila kuwepo mkusanyiko.

 

Serikali, kupitia mamlaka zake za usajili wa katiba za vyama vya michezo, inaiona katiba ya chama cha mchezo wa soka  imepitishwa kwa ukiukwaji, inaelekeza ipitishwe kwa taratibu sahihi. Hapo soka imeingiliwaje na serikali? Nani atarekebisha kosa la TFF la ukiukwaji wa uandishi wa katiba yao? TFF wenyewe wanaoamini hawakukiuka chochote? Lazima kuwe na ‘check and balance’ jamani.

Tusifikie mahali pa kuipa FIFA uwezo wa kuwa kama rais wetu katika masuala yanayohusu watu wa soka. Leo serikali inashughulikia utaratibu wa utengenezaji wa katiba ya chama cha soka (siyo yaliyomo kwenye katiba), madai yanatolewa kwamba serikali imeingilia soka. Kesho mtu wa soka ataiba fedha za chama cha soka, mtasema asichuliwe hatua na vyombo vya serikali kwa sababu FIFA imezuia serikali kuingilia mambo ya soka na mwisho mtu wa soka akimuua mwenzake kwenye mkutano wa chama cha soka mtasema hilo ni suala la soka.

Hebu tuweke mpaka wa mambo ya soka na yasiyo ya soka katika kushughulikia mambo yetu ya ndani ya nchi, ili tusiipe FIFA urais wa nchi yetu katika masuala ya soka. Serikali ya Tanzania ipo sahihi kuhakikisha TFF inapata katiba kwa njia sahihi. Maagizo hayo yapo mbali na soka kwani hayagusi vipengele vya katiba hiyo.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Liverpool watupia Tatu kuwaua Spurs

*FIFA YAWASILISHA KUSUDIO LA KUIFUNGIA TANZANIA*