in , , , ,

England wapigwa teke viwango Fifa


*Cape Verde wapoteza nafasi ya Brazil
* Qatar wanakataa kupokonywa uenyeji

 

Matokeo ya mechi za kimataifa za hivi karibuni yamekuwa chungu kwa England, kwa sababu imeanguka kiviwango kiasi ambacho hakikupata kutokea miaka 12 iliyopita.
England wenye ligi inayopendwa zaidi duniani wameanguka kwa nafasi tatu na sasa wanashikilia ya 17 duniani kwa ubora.
Katika orodha iliyotolewa na Fifa kwa mwezi Septemba inaonesha kwamba wamerudi nyuma ya enzi za kocha Kevin Keegan alipokuwa akiwanoa Simba Watatu hao wa England.
Katika mechi mbili zilizopita, England walishinda mechi moja na kutoa sare nyingine, ambapo waliwafunga vibonde Moldova na kutoka suluhu na Ukraine.
Hispania wanashika nafasi ya kwanza, wakifuatiwa na Argentina, Ujerumani, Italia, Colombia, Ubelgiji, Uruguay, Brazil, Uholanzi na Croatia.

20130913-222504.jpg
Marekani waliofuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia Brazil, wamechupa kutoka nafasi ya 19 hadi ya 13, baada ya kuwa wamecheza zaidi ya mechi 10 bila kushindwa hata moja, wakifundishwa na kocha wa Kijerumani, Jurgen Klinsman.
England wanafundishwa na Mwingereza, Roy Hodgson na mwaka jana walifanikiwa kupanda hadi nafasi ya tatu, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia yake.
Ndugu wengine wa England, Wales wanashika nafasi ya 52, Jamhuri ya Ireland ni wa 59, Scotland wa 63 wakati Ireland Kaskazini wanashika nafasi ya 23.
Hispania ndio mabingwa wa Ulaya, wakiwa wameshinda ubingwa huo mara mbili mfululizo na pia mwaka 2010 walitwaa Kombe la Dunia, na wamekuwa kwenye nafasi ya kwanza kwa miezi 12 mfululizo.

CAPE VERDE KISICHO RIZIKI HAKILIKI

Baada ya kuushangaza ulimwengu wa soka kwa kufuzu kwenye mashindano ya Kombe la Mabingwa wa Afrika msimu uliopita, Cape Verde wamepoteza nafasi ya kucheza mtoano wa mwisho kuingia Kombe la Dunia Brazil mwakani.
Taifa hilo la visiwa vidogo ambalo halikutarajiwa kufanya vyema, liliwafunga Tunisia 2-0 kwao wikiendi iliyopita, lakini Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limewapokonya ushindi huo.
Cape Verde wameponzwa na kumchezesha mchezaji aliyekuwa amefungiwa, Fernando Verela, na sasa Tunisia wamepewa ushindi wa 3-0 na pointi tatu, hivyo kufuzu katika timu 10 bora za Afrika.
Hii imeonesha tena ukosefu wa umakini kwa timu za Afrika, kwa sababu Cape Verde wenyewe walijipatia pointi tatu awali baada ya Guinea ya Ikweta kuchezesha mchezaji aliyekuwa pia amefungiwa.
Fifa imesema kwamba Verela hajamaliza adhabu yake ya kukosa mechi nne baada ya kupewa kadi nyekundu kutokana na vitendo visivyo vya kimichezo dhidi ya mwamuzi.
Chama cha Soka cha Cape Verde nacho kimepigwa faini ya dola 6,400 kwa kosa hilo. Visiwa vya Cape Verde vina watu 505,000 tu, lakini vimekuwa vikitikisa na kuzipita nchi zenye watu zaidi ya milioni 45 kama Tanzania.

QATAR WAKATALIA KUPOKONYWA UENYEJI

20130913-222528.jpg

Qatar imekataa mwito wa kutaka Kombe la Dunia 2022 lihamishiwe nchi nyingine kutoka nchini mwao kwa vile msimu wa kiangazi joto huwa kali kupita kiasi Mashariki ya Kati.
Wadau kadhaa wanataka mashindano hayo yafanyike katika nchi nyingine, kwa sababu wachezaji hawataweza kumudu kucheza katika hali hiyo, na pia washabiki wataugua.

Pamoja na kukataa huko, Fifa inatarajiwa itahamisha mashindano hayo ili yafanyike msimu wa baridi, jambo ambalo si kawaida kwenye ratiba yake.

Rais wa Fifa, Sepp Blatter alishasema anadhani kwamba ilikuwa makosa kuamua mashindano hayo kufanyika Qatar katika majira ya kiangazi.

Zipo tuhuma nyingi na nzito kwamba mlungula ulitumika katika kuhakikisha mashindano yanafanyika nchini humo, zinazodaiwa kutolewa na mashirika makubwa yanayofadhili soka nyumbani humo na hata Ulaya.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka England, Greg Dyke alisema anadhani mashindano hayo yatahamishiwa nchi nyingine ikiwa hayatapatikana majira mbadala ya kucheza nchini Qatar.

Lakini Mkuu wa Maandalizi ya Kombe la Dunia Qatar 2022, Hassan al-Thawadi anasema hakuna sababu toshelezi kwa nini Qatar wasiandae mashindano hayo, kwani walifanya kazi ya ziada kuhakikisha wamo ndani ya sheria na kanuni za kupata uenyeji na wameshafanikiwa.

Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu ya England, Richard Scudamore anasisitiza kwamba lazima mashindano hayo yafanyike majira ya kiangazi kama ilivyo kawaida, hivyo kuwapo uwezekano wa kuhamishwa kutoka Qatar.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Ulaya (Eca), Karl-Heinz Rummenigge, anasema pengine ni vyema zaidi kufanya mashindano hayo majira ya baridi.
Eca ni chombo huru kinachowakilisha maslahi ya klabu kubwa za Ulaya. Klabu 10 za England ni wanachama wake, nazo ni Arsenal, Aston Villa, Chelsea, Everton, Fulham, Liverpool, Manchester City, Manchester United, Newcastle na Tottenham Hotspur.

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Italia, Uholanzi zafuzu Kombe la Dunia

Pigo la kwanza kwa Mourinho