in , , ,

Bert Trautmann na soka la Tanzania, alituwekea msingi…..

WIKI hii ulimwengu wa soka umempoteza mmoja wa wataalam wa soka waliobobea, Mjerumani Bert Trautmann aliyefariki dunia Ijumaa ya Julai 19, 2013 jijini Valencia nchini Hispania alikoamua kuweka makao yake baada ya kustaafu shughuli za soka. Amefariki akiwa na umri wa miaka 89 akikaribia miaka 90 kwani alizaliwa jijini Bremen, Ujerumani Oktoba 22, 1923. Msiba huu unatugusa Watanzania kwa sababu mtaalam huyo alikuwepo nchini mwetu mwaka 1975 katika kutimiza mpango maalum wa FIFA wa kutuma wataalam wake kuinua soka kwenye nchi zilizokuwa chini kisoka.

Alianzia kutekeleza mpango huo Burma (1972-1974), akawa kwetu (1975), kisha akaenda Liberia (1978-1980) na kumalizia mpango huo Pakistan (1980-1983). Inaelezwa kuwa kutokukaa sana hapa kwetu kulisababishwa na ugunduzi wake kwamba kisoka hatukuwa chini kihiiivyo kabisa kwa hiyo alishauri aende maeneo hasa yaliyokuwa hoi kabisa kisoka. Usishangae kuona Liberia alikaa kwa muda zaidi ya hapa. Walikuwa chini yetu hao na ukweli ni kwamba hata sasa hawatuwezi.

Bert Trautmann, ambaye jina lake halisi ni Bemhard Carl Trautmann, alikuwa mchezaji maarufu wa Manchester City kati ya mwaka 1949 na 1964 akicheza mechi 508 katika nafasi ya ukipa aliyokuwa akichezea. Cha kusisimu, akiwa hapa kwetu alitengeneza timu ya makipa hodari tupu, Athumani Mambosasa na Omar Mahadhi wote kutoka Simba ambao kwa sasa ni marehemu. Aidha, alimuibua kijana mdogo wa wakati huo, Juma Nassor Pondamali na kumfanya kuwemo kwenye timu ya taifa kukamilisha orodha ya makipa watatu hodari tupu-Mambosasa, Mahadhi na Pondamali. Hii isitafsiriwe kwamba utaalam wake hapa ulikuwa zaidi kwa makipa, hapana, Trautmann, kama mtaalam wa soka, alifundisha mbinu za mpira kwa nafasi zote akitupia macho umuhimu wa vipaji vya vijana na kutoa elimu kwa makocha wetu wa wakati huo hasa Joel Bendera aliyekuwa msaidizi wake na wengine kama kina Mohammed Msomali. Joel bendera kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Kwenye kuwaamini vijana, mbali ya Pondamali, aliwainua kina Mohammed Salim wa Coastal Union ya Tanga, Omari Hussein, Aluu Ali na Hussein Ngulungu wa Mseto ya Morogoro na vijana wengine waliochipuka tu mwaka huo 1975 na mwaka mmoja kabla. Ni kocha huyo ndiye aliyeona kuwa Mohammed Kajole wa Simba (marehemu) ndiye aliyestahili kuziba pengo la beki ya kushoto lililoachwa wazi na Mohahammed Chuma wa Nyota ya Mtwara aliyestaafu kuchezea timu ya taifa mwaka huo baada ya kuichezea mfululizo tangu mwaka 1964. Kama tulivyoeleza majuzi, Kajole aliitwa kujiunga na wenzake Zambia kwenye mashindano ya Challenge ya mwaka huo.

Tuna kila sababu za kumkumbuka kocha wetu Bert Trautmann kwa sababu msingi wa soka aliouweka uliimarishwa vizuri na waliompokea jukumu la kuifundisha timu yetu ya taifa kwani miaka minne baadaye, 1979, tulifanikiwa kukata tiketi ya fainali ya mashindano ya mataifa (huru) ya Afrika nchini Nigeria, tuliyoshiriki mwaka 1980.

Katika historia ya maendeleo ya soka yetu, Watanzania hatupaswi kumsahau Trautmann kwani alichangia kwa kiasi kikubwa kutuinua kisoka. Mungu amlaze pema peponi mtaalam wetu wa soka Bemhard Carl Trautmann, maarufu kama Bert Trautmann.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

MAELEZO YA SHUKURANI YA MWENYEKITI ALIYEMALIZA MUDA WAKE WA KAMATI YA UCHAGUZI YA TFF – KWA VIONGOZI NA WADAU WA SOKA NCHINI

CAF yateua waamuzi wa Taifa Stars dhidi ya The Cranes