in , , ,

ADHABU ZIWE DHIDI YA WACHEZAJI MOJA KWA MOJA

MWAKA 2007 mchezaji Athumani Idd wa Yanga aliponyoosha kidole cha kati kwa mashabiki wa Simba kwenye mashindano ya kombe la Tusker ndani ya uwanja wa Kirumba jijini Mwanza, kamati ya mashindano hayo iligwaya kumuadhibu mchezaji huyo ikijua kwamba kufanya hivyo kungeiudhi Yanga! Walichoamua ni kumuonya na kuielekeza klabu yake imuonye asirudie tena upuuzi huo. Uongozi wa Yanga uliahidi ungemuonya vikali mchezaji wao huyo na mchezo ukaonekana kumalizika hivyo lakini Rais wa TFF, Leodgar Tenga akabadili upepo na kuagiza lazima mchezaji huyo aadhibiwe kulinda hadhi ya mchezo wa soka.

Kwa nguvu ya agizo hilo, mchezaji huyo akafungiwa kushiriki mechi za timu yake zilizobaki za mashindano ya Tusker ya mwaka huo. Cha ajabu baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, viongozi wa Yanga wakaja juu kwamba mchezaji wao huyo alikuwa ameonewa kwa sababu alifanya alivyofanya baada ya kuchokozwa na mashabiki wa Simba. Hawakuishia hapo, hata kwenye kupokea kombe la ubingwa walimteua mchezaji huyo aliyefungiwa kuwa ndiye wa kupokea kombe! Viongozi hawa ndiyo eti wangemuonya mchezaji kwa utovu wa nidhamu. Kwa Tanzania hiyo ni ndoto. Viongozi wengi wa soka wa Tanzania wanawadekeza mno wachezaji wao hata wanapofanya mambo mabaya ya kiwango kisichomithilika.

Mahakama

Inakuwaje klabu moja inaongea na mchezaji kuhusu kuingia mkataba naye, mchezaji anawahakikishia hana mkataba na klabu yoyote nyingine kwamba yeye ni huru,inaingia mkataba naye kisha ghafla inaibuka klabu nyingine na kuonesha mkataba halali kwa kila kitu na mchezaji huyo? Mchezaji anahukumiwa kwa ujinga alioufanya, klabu ya pili kuingia mkataba naye inakata rufani kupinga adhabu hiyo! Maelezo ya rufani eti mchezaji kaonewa au kapewa adhabu kubwa!

Mchezaji anafanya utovu wa nidhamu wa hali ya juu akiitumikia timu ya taifa, anaadhibiwa,klabu yake inakuja juu kulalamika eti kaonewa na eti mchezaji huyo hana tabia za utovu wa nidhamu! Sasa hivi umezuka mtindo wa wachezaji wa Tanzania kuchukua pesa za usajili toka klabu mbili kwa kusaini kabisa mikataba. Wanafanya hivyo wakiamini makubaliano yatafanywa baina ya klabu husika kisha wao watahalalishwa kuchezea timu ya klabu ya pili kuingia nayo mkataba, iliyotoa pesa nyingi! Hawana hofu kabisa ya jambo hilo kwa sababu wanajua hakuna adhabu ya faini watakayolazimika kuilipa kibinafsi.

Ramadhani Chombo na Mbuyu Twite walipoingia katika tatizo hilo, klabu za pili kuwapa pesa, Simba kwa Chombo na Yanga kwa Twite zililazimishwa kurudisha pesa kwa klabu za kwanza kuwapa pesa za Azam kwa Chombo na Simba kwa Twite kutokana na amri ya wachezaji hao kurudisha pesa hiyo. Wachezaji hao hawakulalamika kabisa kwani walijua wa kurudisha pesa hiyo alikuwa si wao bali zile klabu za pili.

Kwa msingi huo huo haishangazi Mrisho Ngassa hivi karibuni kulalamikia adhabu ya kukosa mechi sita za msimu huu wa ligi kwa kosa la kuchukua pesa za Simba na za Yanga akikusudia kuichezea Yanga. Kwake yeye kukosa mechi sita ulikuwa mzigo mzito kuliko kurudisha shilingi milioni 45 kwa Simba! Anajua wazi kuwa licha ya yeye kutakiwa kulipa pesa hiyo, Yanga ndiyo watalipa.

Ili kukomesha vitendo vya utovu wa nidhamu na udanganyifu kwa wachezaji wa Tanzania, kwanza, klabu zetu zisiwe watetezi wa wachezaji watovu wa nidhamu na wadanganyifu kama tuna viongozi wa kweli wa soka. Pili, TFF inapotengeneza kanuni za kuadhibu wachezaji wanaokiuka taratibu mbali mbali wasiwe na mtazamo tofauti inapotokea wachezaji wa Yanga na Simba wanakiuka taratibu kwa mujibu wa kanuni.

Hebu angalia, mchezaji anaingia mikataba na timu mbili kuzitumikia kwa kipindi kimoja. Huu ni udanganyifu mkubwa na mbaya sana ambapo adhabu yake kwa mujibu wa kanuni ni kufungiwa kucheza kwa msimu mmoja lakini anafungiwa mechi sita tu ambazo ni takriban mwezi mmoja na nusu tu. Mchezaji huyu alipaswa ashukuru kwa kupewa adhabu ndogo iliyo tofauti kwa mbali na uzito wa kosa alilotenda lenye adhabu kubwa kuliko hiyo. Kinyume chake analalamika kwa sababu alijua kwamba alikuwa hastahili adhabu yoyote si kwa sababu hakutenda kosa bali kwa sababu hii ni Tanzania na mchezaji huyo anaihusu Yanga!

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) kosa la klabu kuingia mkataba na mchezaji mwenye mkataba na klabu nyingine ni klabu hiyo kuzuiwa kununua wachezaji wapya kwa misimu kadhaa. Hivyo, klabu yetu hii ya Tanzania ilipaswa ishukuru kwa suala la mchezaji huyo kumalizika kilaini hivyo kwa upande wao tena kwa kupewa uhalali wa kummiliki mchezaji waliyempata kwa kuvunja kanuni lakini kinyume chake klabu hiyo inalalamika na kupanga kukata rufani! Hii inasababishwa na klabu hiyo kuwa ya Tanzania na kuwa moja ya klabu zinazoogopwa.

Wakipata mshauri mzuri wanapaswa washaurike kuikubali fadhila waliyopewa na TFF, wakiliendeleza suala hili hadi likafika kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kesi za Michezo (CAS) wanaweza kuangukiwa na rungu baya kwani watu wa CAS wanachojua ni kanuni tu; hawajui Yanga wala Simba.

Jambo la tatu la kuzingatiwa ili kuwafanya wachezaji wetu kukaa kwenye mstari sahihi wa nidhamu na kuacha udanganyifu ni kupewa adhabu zitakazowaumiza moja kwa moja kama kufungiwa kwa muda mrefu kwa makosa hayo ya makusudi kabisa wanayoamini adhabu zake zitaziumiza klabu zinazowadekeza na wala si wao. Adhabu hizo ni za faini kwao ambazo hulipwa na klabu, tofauti na huku Ulaya wanakolipa wachezaji wenyewe.

Kwa njia hizi wachezaji wa Tanzania wataacha udanganyifu na watajiepusha na utovu wa nidhamu hata wakiwa wa Yanga na Simba. Hebu tuache utani utani katika masuala nyeti na mazito kama ya uendeshaji wa soka yetu. Na waandishi wa michezo wa nyumbani msiwapotoshe watu kuwaelekeza kusiko na ukweli. Mchezaji akiwa huru tayari kuongea na klabu yoyote kwa ajili ya kuingia mkataba naye, klabu aliyokuwa akiichezea kwa mkopo haiondolewi kikanuni kuongea na mchezaji huyo akiwa huru tayari; akiwa hana timu yoyote. Hoja ya Simba kuwasiliana na Azam kabla ya kuingia mkataba na Ngassa inasimama tu kama Simba wangefanya hivyo wakati mchezaji huyo akiwa bado wa Azam

Kama Mrisho Ngassa alikuwa tayari huru kuongea na Yanga bila ya Yanga kuwasiliana na Azam, kwa nini tulipotosha kwamba Simba ilikuwa haina uwezo wa kuongea naye katika kipindi hicho hicho bila kuwasiliana na Azam? Mchezaji huyo alikuwa huru kwa wote na aliyetangulia kuingia mkataba naye ndiye alikuwa halali kummiliki. Tuwe tukifanya utafiti kabla ya kuandika kishabiki. Ngassa kisheria alikuwa halali kwa Simba lakini alipenda kuichezea Yanga na kufanya kosa la kuingia mikataba na zote na alistahili adhabu kubwa.

Adhabu za makosa ya wachezaji wa soka wa Tanzania sasa ziwe za kuwaumiza wachezaji moja kwa moja ili waache udanganyifu na wajiepushe kuwa watovu wa nidhamu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Mathieu Flamini arejea Arsenal

TFF, AZAM MEDIA ZASAINI MKATABA WA BIL. 5.5/-