Makala
Kama mkazi wa Dodoma , huko nyuma nimemshuhudia Mhe Kikwete, akishiriki katika michezo mbalimbali kwa nyakati tofauti, kwangu mimi mifano mingi itakuwa ni awapo Dodoma .
Kufuatia Vikao vya bunge na mikutano mingi ya CCM, kufanyika Dodoma , ni rahisi kufahamu ,baadhi ya viongozi wanapenda nini baada ya saa za kazi au wanajishirikisha vipi na maisha ya kijamii (Socializing) kufuatia mimi kuwa kiongozi wa michezo katika ngazi ya mkoa, nilibahatika kuwa karibu na kiongozi huyu, katika baadhi ya majukumu yake ya michezo awapo Dodoma .
Japo ukaribu wangu ni wakuwa naye katika meza moja na sikuwahi kuongea naye, kwani mara nyingi nilikuwa nawekwa mstari wa nyuma kabisa huku yeye akiwa mstari wa mbele kama kiongozi, hii ni kazi ya meneja wa uwanja wa jamuri mjini Dodoma , Bw Jaffari Mwanyemba.
Katika moja ya matukio ya Mhe Kikwete na mambo ya michezo ni pale alipoongoza mkutano mkuu wa chama cha mpira wa kikapu Tanzania , (BATA), mjini Dodoma katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, mpaka saa nane usiku! ,ulikuwa ni mkutano muhimu kwa maendeleo ya mpira wa kikapu, naye kama mlezi alihakikisha anashiriki na kutoa maonyo kwa viongozi waliokuwepo, hawa ni pamoja na Jackson kalikumtima, Saleh zonga, Fred ogot, Simba na wengi wao, huku akionyesha kutoridhika kwake na jinsi kasi ya maendeleo ya mpira wa kikapu inavyofunikwa na migogoro na kutoelewana kwa viongozi (miaka mitatu iliyopita), kwangu mimi kama kiongozi wa mpira wa wavu, niliona wivu sana, na kujiuliza mbona sisi hatuna mtu wa kutuongoza pale tunapokwama,, hata kupelekea maendeleo ya mpira wa wavu nchini kufifia huku chama cha mpira wa wavu (TAVA), kupitia kwa mwenyekiti wake, Agustino Agapa kukiri hivi karibuni kuwa mambo si shwali ndani ya TAVA.
Inatia moyo sana unapokuwa na kiongozi wa ngazi ya juu katika serikali , anapoonyesha kujali na kuwajibika katika maendeleo ya michezo nchini mwake, nilifarijika sana jinsi alivyoongoza mkutano na uvumilivu wa kukaa mpaka usiku wa manane, pale mkutano ulipoisha.
Pia amekuwa akishiriki katika michezo mingine kama Netiboli, na haswa kwenye mashindano maarufu ya Kumbukumbu ya Hayati Mwalimu Nyerere, yakijulikana zaidi kama, Nyerere cup, Yalikuwa yakifanyika kila mwaka mjini Dodoma . Pia Mhe Kikwete, amekuwa akishiriki katika burudani pale anapopata muda, haswa baada ya kazi awapo mjini Dodoma, na kwa maana hiyo, yeye sio mgeni sana na kumbi kama Kilimani Club, Dodoma Hotel,Dodoma Inn, nk, kila kukiwa na muziki wa Dansi, kadhalika ni mshiriki mkubwa wa Mnadani kila jumamosi akiwa na jamaa na marafiki zake, huku akitumia muda mwingi kuzungumza na wananchi wa kawaida.
Ni imani yangu kuwa Mhe Kikwete, anatambua hali mbaya ya michezo nchini, hii ikiwa ni pamoja na usimamizi mbovu wa michezo, unaopelekea nchi kutajwa zaidi nje ya nchi kwa sababu za kisiasa kuliko michezo, tofauti na miaka ya nyuma, ambapo Tanzania ilijulikana na kutajwa sana , kama nchi anayotoka Filbert Bayi, Juma Ikangaa, Nzael Kyomo, Sunday Manara, Mohamed Chuma, Zamoyoni Mogella, William Isangura, Gidemus shahanga, Familia ya Matumla na wanamichezo wengi, waliokuwa tayari kupoteza maisha yao wakitetea jina zuri la Tanzania, hapa namzungumzia John Stephen, pale alipomaliza mbio zake nchini Mexico, akiwa wa mwisho, huku akiwa ameumia, nakuuambia umati wa waandishi wa habari kuwa Watanzania wamemtuma kumaliza mbio na sio vinginevyo, huo ni ushujaa wa aina yake, hatuna tena wanamichezo kama hawa, huku ubora wa maisha ukiwa umeimarika zaidi, viwanja ni vizuri, wataalamu wa michezo wanapata mafunzo yalio bora, sayansi na teknolojia imeshamiri duniani kote, na hivyo kujua tabia au kiwango cha mpinzani wako, hata kama yuko mbali kiasi gani, na hivyo kujiandaa kikamilifu.
Tanzania kwa sasa hatuna Mwanamichezo ambaye tunaweza tukasema ni Balozi wa Nchi, kwa maana ya mafanikio yake kuigwa na wanamichezo wengine nchini, na hivyo kupelekea kuwa mfano wa kuigwa na wanamichezo wadogo wanaochipukia (Icon), tumekuwa tukijivunia na mashindano ya uzuri na kuwatumia warembo kama mabalozi wetu, sawa, lakini ni kwa kiasi gani, tutafanikiwa bila kuwashirikisha wanamichezo wetu, ambao wanaoanisha akili zao, miili yao na kufikia viwango vya juu kabisa katika ushindani wa kimataifa, huku Taifa zima likisisimuka nyuma ya Mwanamichezo huyu, na kujivunia kuwa Mtanzania popote ulipo Duniani.
Nchi nzima imeathirika na uamuzi wa waziri wa Elimu na Utamaduni, Mhe Joseph Mungai, kwa kuyafuta mashindano ya Umitashumta na Umiseta kwa ngazi zote nchini, amekuwa akijitetea kuwa uamuzi wake unalengo la koboresha zaidi , kiwango cha Elimu, na kuwa hajawazuia wanafunzi kushiriki michezo, lakini anasahau kuwa kushiriki michezo bila kushindana ni sawa na hao wanafunzi kusoma mwaka mzima na kisha kuwapa vyeti vya kuhitimu, bila kufanya mitihani!
Kufuatia maamuzi haya mabaya nchi haina utaratibu wa kupata wachezaji wapya, vipaji vinaishia vijijini kwani vijana hawana jinsi ya kusafiri na kushiriki michezo katika sehemu nyingine za nchi, kufuatia umasikini wa wazazi wao,na vijana wamepoteza nafasi ya kuijua nchi yao kijiografia, kwani mashindano haya yalitoa nafasi kwa kila mkoa kaandaa mashindano kwa kipindi fulani, na hivyo kutoa nafasi kwa wanafunzi na walimu wao kusafiri sehemu mbalimbali za Tanzania na hivyo kuijua nchi yao .
Pia wataalamu wa michezo wamekuwa wakifanyia kazi zao katika mazingira yale yale, kwani hakuna ushindani wa kutosha, pia timu zimekuwa chache sana katika mashindano mbalimbali, na hivyo kupelekea vyama vingi vya michezo kitaifa, kukwama kuendesha kazi zao hata kupelekea kalenda zao, kuwa na mapungufu makubwa katika kufikia malengo yao ya kiutendaji, hii ni pamoja na mafunzo ya waamuzi wapya, na mambo mengine ya kiutendaji na ufundi.
Natambua kuwa kulikuwa na mapungufu mengi katika uendeshaji wa michezo ya Umitashumta na Umiseta , kwa mfano: usafiri kwa wanafunzi haukuwa mzuri,hata kupelekea ajali iliyopoteza maisha ya mwanafunzi mmoja akitokea michezoni kondoa, usimamizi wa michango inayotolewa na wazazi kuliwa na baadhi ya walimu wasio waaminifu, chakula kuandaliwa katika mazingira yasio bora kwa afya ya wanafunzi na walimu, haya yote yalitakiwa yafanyiwe kazi na mapendekezo yapelekwe kwa wahusika ili michezo hii iboreshwe na sio kuifuta kwa kuamini kuwa, kwa kufanya hivyo, vijana wote watafanikiwa katika elimu.
Tanzania tuna amani, nchi yetu ni nzuri, mazingira yanaruhusu kwa mchezaji yeyote kufanikiwa katika mchezo anaoupenda, ajabu ni kuwa hatuna mchezaji hata mmoja kwenye ligi kubwa Duniani, kuna nchi zenye migogoro kwenda mbele!, nabado zimefanikiwa kujiingiza katika soko la michezo na wachezaji huku ulaya, huku uchumi wanchi zao ukikuwa na kijitangaza kwa mafanikio yao, huku sisi tukibaki tukijitetea kuwa tuna amani, tulikuwa na Juma Ikangaa, tulikuwa na Juma Pondamali, na wengi wengineo, nchi inatajwa zaidi kwa mambo mabaya kwenye vyombo vya habari vya huku ulaya, sisi ni moja kati ya nchi masikini zaidi duniani, limeandika gazeti la udaku la The Sun, Rais wetu ana ndege ya gharama zaidi, ukimwi unatumaliza, Rushwa imekithiri kwa viongozi wetu, nk.
Inaudhi zaidi pale unapopoteza muda mwingi kujitetea mbele ya wanafunzi wenzako toka nchi mbalimbali duniani, na huku ukiulizwa ni mchezo gani maarufu Tanzania, au ni mchezaji gani aneyechezea timu za kulipwa toka Tanzania, Kwani wanategemea kama kweli mna amani na utulivu, na Bendera yenu haina rangi nyekundu kuashiria kuwa hamkumwaga damu ili kupata uhuru wenu, basi nyie ni bora kabisa katika manbo ya jamii hii ni pamoja na michezo.
Tunahitaji kubadilika, michezo ipewe kipaumbele, tuwe na wanamichezo wetu, tuwapende na kujivunia, timu zetu za vijana wadogo zishiriki mashindano nje ya nchi, Elimu na michezo iende sambamba, kwani nani anajua kiwango cha Elimu cha David Beckham, Thiery Henry, Michael Owen au Ronaldo..
Hawa ni matajiri na walianzia michezo mchangani, kuna watu wenye akili wakawaangalia, wakawapa nafasi ya kushiriki michezo, na sio kuwakatisha tamaa kwa kuwalazimisha kutumia muda mwingi darasani huku, mawazo ya mwanafunzi yako uwanjani, tufike mahala tuheshimu, utashi wa vijana wetu, na kuwapa mwongozo (Guidance), kwa yale mema wanayoelekea kuyapendelea na kuwaweka kwenye mstari wanapokosea.
Mwisho kwako mheshimiwa Kikwete, endapo utachaguliwa na kuingia ikulu, tafadhali tunakuonba uturudishie heshima yetu katika michezo na wachezaji, Tanzania haistahili kuwa hapa ilipo kwenye mambo ya michezo., tunastahili kuwa juu zaidi katika ramani ya michezo Duniani.


